WAKATI umefika sasa kwa Watanzania kurejea katika mifumo ya utawala tuliyorithi na kujiuliza kama inatufaa.
Matukio ya hivi karibuni yaliyotokea bungeni ambayo wabunge walitaka kuiangusha Serikali kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani, ni ishara inayoonyesha kwamba mambo si shwari. Mfumo wa sasa wa mawaziri kutokana na wabunge siyo tu unatwisha mzigo wa ziada wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanatakiwa kutumika katika mihimili miwili ambayo ni utungaji sheria na utawala. Wakati mwingine inaonekana rahisi kwa wabunge kupitisha hukumu, kukejeli na hata kudharau kazi inayofanywa na watu wengine wakiwa ni watendaji serikalini na mawaziri. Yawezekana kabisa kwamba wako watendaji na viongozi wajanja wanatambua udhaifu na upungufu katika mfumo wetu wa uongozi na utawala wa nchi. Na hivyo wanajinufaisha wenyewe na kutanguliza ubinafsi.
Lakini kuna ukweli usiopingika kwamba matatizo ya kisheria, miundo na mifumo yetu ni mikubwa, kiasi kwamba hata wakipewa nafasi ya kuteua mawaziri wanaowataka, baada ya muda hao wateuliwe wao watakumbana na vikwazo katika utendaji kazi wao. Kwa mtu asiye na tamaa ya uongozi (asiye na uwezo) ni heri akae pembeni akiwa mwakilishi kuliko kuteuliwa waziri.
Hebu tufikirie Waziri wa Nishati na Madini. Sasa hivi hakuna matatizo ya maji katika mabwawa kwani mvua zimenyesha na maji yamejaa. Lakini bado umeme unakatikakatika kwa sababu miundombinu ya kusambaza umeme imeishaoza. Tanzania haikuwa na utamaduni wa kutenga fedha kukarabati umeme. Huo ni mfano mmoja kati ya mifano mingi. Kuna mifano ya sekta ya umma kuwapoteza wataalamu wake. Kwa sekta binafsi na mashirika ya wafadhili, madaktari na mainjinia wanakimbilia nchi za nje kutafuta maisha. Hali hiyo inazorotesha huduma. Lawama zinakwenda kwa waziri mwenye dhamana.
Kwa upande mwingine bunge ambalo sasa linan