HIVI karibuni, Tanzania ilikumbwa na mgomo wa madaktari ulioitikisa nchi kwa kiasi cha kutisha. Madaktari waligoma wakitaka madai yao kadhaa yatekelezwe na mwajiri ambaye ni Serikali.
Ninaandika makala haya nikijua kuwa suala la mgomo wa madaktari liko mahakamani hivyo, siwezi kuzama hadi uvunguni kulizingumzia na badala yake, niiachie Mahakama ifanye kazi yake ya kugawa haki.
Hata hivyo, nipende tu kusema kwamba, ingawa mgomo huo ulisababisha madhara kwa jamii na hususan wagonjwa walioteseka na wengine kupoteza maisha, hatukuona kituko cha hatari kama hiki ambacho jamii ya Watanzania imekishuhudia hivi majuzi kaika mgomo wa walimu.
Hatukuona madaktari wakiwashirikisha wateja wao; wagonjwa katika mgomo wala kuwatuma kufanya maandamano ili eti serikali ione athari na kuamua kushughulikia madai yao.
Katika hali ya kushangaza, walimu ambao ni tegemeo la umma katika kufinyanga akili za watoto shuleni, wamelifanya hilo.
Walimu wameona hoja zao, sauti zao na mazingira yao labda yanapwaya; wameamua kuwachukua wateja wao ambao ni wanafunzi; tena watoto wao na kuamua kuwashirikisha katika mgogoro baina yao (walimu) na mwajiri wao ambaye ni Serikali.
Binafsi nimejiuliza bila kupata jibu kwamba, walimu wamefundishwa na nani mtindo huu mchafu na hatari wa kuua akili za watoto wa Kitanzania kikatili namna hii? Hivi walimu ambao pasi na shaka baadhi yao walikuwa wagonjwa wakati wa mgomo wa madaktari, wangewezaje kushiriki na wangejisiakiaje kutumwa na kushinikizwa kunyanyuka wodini katika vitanda vya wagonjwa, ili waende kuandamana?
Ieleweke kuwa, makala haya hayalengi kuwalaumu walimu kwa kudai maslahi yao ili wafanye kazi wakiwa katika amani ya akili na hivyo, kufanya kazi kwa utulivu na moyo wa ufanisi, la hasha, hiyo ni haki yao lazima waidai ili wautumikie vyema umma kupitia kazi na wito wao.
Hii ni kwa sababu, umuhimu wa walimu ni ule usioweza kumithilishwa na mtu mwingine yeyote maana bila mwalimu, taifa litaongozwa na watu gani wasiojua kusoma wala kuandika; wenye upeo mdogo wa kuyatazama mambo; bila walimu, tunapataje madaktari; tunapataje wachumi; tunapataje wanasiasa safi tunawapataje hata viongozi wa dini wanaojua kuchambua mambo na hata kuwalea watu kiroho na kimwili!
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba ya mwisho Julai mwaka huu, alisema, “Napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu. Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo mbalimbali isipokuwa, madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo.”
Ukiacha dosari za kisheria zilizoifanya mahakama kutengua mgomo wao, niseme wazi kwamba makala haya hayalengi kujadili chanzo, uhalali, au kuwa msaidizi wa mahakama katika kuhukumu upande wowote wa mgogoro baina ya Serikali na walimu kupitia (CWT), bali imelenga kuyatazama madhara ya mgomo huu kwa watoto wa Kitanzania yaani, wanafunzi kama zao la ukosefu wa umakini au basi ukosefu wa nia njema kwa walimu.
Kimsingi, mgomo huo umesababisha athari kubwa katika mfumo wa utoaji elimu nchini kuanzia msingi na sekondari na hasahasa, kwa watoto wanaotarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa wakiwamo wa darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na hata wa kidato cha sita.
Mgomo huu uliopangwa kipindi hiki cha darasa la saba kuelekea mitihani yao ya taifa kwa vyovyote, kimechangia kwa kiasi kikubwa, kumewaharibia watoto hawa maisha yao yote duniani na ndiyo maana, busara za uzazi zilihitajika kabla ya mgomo huu.
Walimu walipaswa na naamini kuwa walijua kabisa kuwa kitendo chao cha kuvizia mitihani ikaribie eti ndipo wagome kama njia ya kuikomoa Serikali, si kweli kwamba kililenga hivyo tu, bali hasa kuwakomoa wazazi na watoto wao wanaoelekea mitihani ya taifa hivyo, ni kitendo kisicho cha kizalendo tena kisichosameheka hivi hivi.
Ninasema busara kwa sababu wana madai yao ambayo uwezo wa Serikali ni mdogo kuyatimiza yote na wakati huohuo, madhara ya mgogo (mgomo) huu yanawagonga watoto ambao sio sehemu ya mgogoro.
Kilichonishangaza na kunisukuma kuandika makala haya, ni namna Rais wa CWT, Gratian Mkoba alivyonukuliwa akijivunia kufanyika kwa mgomo huo akisema, umekuwa wa mafanikio makubwa, kwa kuwa umehusisha asilimia 95 ya walimu na kwamba, walimu wachache wanaoendelea kwenda shuleni ni waoga, wanafiki na wenye kujipendekeza kwa mwajiri ili wapate vyeo kupitia kuwasaliti wenzao wanaodai haki zao.
Tofauti na madaktari ambao nao walihiari kuona majeneza yanagombaniwa kutokana na ongezeko la vifo walivyopika kutokana namgomo wao, katika taarifa zote za mgomo sikuwasikia wakijivunia mgomo wao ingawa wagonjwa walikuwa wanateseka na hata wengine wanakufa.
Kujivunia mafanikio ya mgomo kwa madaktari, kungemaanisha kwamba wagonjwa wasio na kosa wala wasio sehemu ya mgogoro, wameteseka na kuugua na hata kufa zaidi. Madaktari walikaa kimya na kubwa zaidi, mara kadhaa walisema wanasikitishwa na hali inayowakumba wagonjwa ingawa kusema tu, huku watu wanateseka na kufa hakuna maana.
Kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam kiliwanukuu baadhi ya watoto wa shule za msingi jijini humo wakieleza namna walivyoshawishiwa na kusukumwa na walimu wao kufanya maandamano.
Kadhalika, zipo taarifa kuwa wanafunzi katika shule kadhaa walihamasishwa na hata kushinikizwa kuwafuata walimu hao wakati wakiandamana kwa kuwatangulia mita kadhaa mbele ili walimu hao wasibainike wazi.
Lakini wapo waliovuka mpaka kwa kushinikiza wanafunzi kuandamana na wengine kufanya uharibifu kwa majengo ya shule na mali nyingine ambazo si za walimu, bali ni za mwajiri ambaye ni Serikali.
Mbaya zaidi baadhi ya walimu wakashambulia wenzao waliokataa kugoma! Ilidhihirika wazi kwa baadhi ya wanafunzi kuonyesha kupata mafunzo kutoka kwa watu wasiojulikana na kuandaa barua na kwenda mahakamani eti kufungua mashitaka dhidi ya Serikali wakipinga kunyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Kwingineko wanafunzi wakionyesha pia kufunzwa, walikusanyika na kuimba: “Tunataka haki yetu! Tunataka haki yetu!” wakiwamo hata watoto ambao ni dhahiri hawajui mgomo ni nini na una malengo gani.
Hapa, walimu wamewakosea Watanzania na hii inadhihirisha wazi kuwa inawezekana pamoja na kugoma sasa, ni dhahiri kuwa kipindi chote cha nyuma walikuwa wamegubikwa na maandalizi ya mgomo huo huku wakitoa mafunzo kwa wanafunzi wao kuandamana, kuimba na kuharibu mali za umma.
Hawa, ni walishaanza kugoma muda mrefu na waliutumia kwa masuala ambayo hayana tija katika tasnia ya elimu, bali uchochezi na kujenga chuki dhidi ya Serikali.
Safari hii, nimeiona tofauti kwa walimu; walimu wa watu; kioo na wafinyanzi wa maisha ya jamii. Walimu kupitia Rais wao, Mkoba, wanajivunia mafanikio ya mgomo yaani, kutofundishwa wanafunzi. Wameshindwa kukumbuka kuwa mafanikio ya mgomo siku zote ni maumivu kwa watumiaji wa huduma za wagomaji.
Rais huyo wa walimu amenukuliwa akidai kuwa walimu hao wanaoendelea na kazi, ndio wamekuwa wakisababisha vurugu kwenye baadhi ya shule kwa sababu wao (CWT) wamewaagiza walimu kubaki nyumbani.
“Tunawaagiza walimu waendelee kubaki majumbani kwani wanaweza kusingiziwa na mwajiri kwamba wanawachochea wanafunzi kuandamana na kuharibu vifaa vya shule,” amenukuliwa akisema na huu ndio msingi hasa wa makala haya.
Walimu wamewakosea watoto na Watanzania kwa kuwatumia watoto katika migomo na maandamano ili kudai maslahi nahii sio kuwatendea haki watoto, bali kuwasaliti watanzania waliowapw dhamana ya kulea watoto wa taifa hili.
Huu ni ukatili wa kuwajengea watoto wetu kasumba hatari ya kutumia migomo na maandamano kama njia ya kuomba kila kitu. Hauna tofauti na kuwashirikisha watoto katika vita; ni ukatili wa kutisha dhidi ya watoto.
Mtindo wa ajabu na hatari wa walimu kugoma na kuwashirikisha wanafunzi katika mgogoro na kwa kile ninachokiona kuwa ni makusudi, wakaacha kuweka mazingira salama kwa watoto (wanafunzi) badala yake, watoto wakitumbukizwa katika shimo la mgogoro ili wafanye wasichokijua; matokeo yake, wengine sasa wanaugulia maumivu na madhara ya aina mbalimbali baada ya kushirikishwa katika hicho walimu wanachokiita kudai haki, lakini ndani yake kuna sura ya kisiasa zaidi kuliko kitaaluma.
Walimu walioweka pembeni taaluma yao na kujiingiza katika siasa kimyakimya na kuanza kuambukiza watoto tunaodhani dhamana waliyopewa ya kuwalea, ndiyo ingetumika kuliko matarajio ya kisiasa, wamulikwe na wauambie umma mbele ya mahakama kuwa walilenga nini kwa watoto.
Nashindwa kuamini kama kweli walimu ndio wamefanya hili la kuwashinikiza wanafunzi katika mgomo kwa staili ya kutuma kimyakimya kufanya maandamano na wao kujiweka pembeni kama wasiojua kitu,
Nasema hivyo kwani walimu wanayafanya haya, wakijua kabisa hasara ya hali, akili na mali wanayoisababisha kwa jamii ya Watanzania na wanajua kabisa kwamba, wao wenyewe walipaswa kuufundisha umma kuwa, uchu na matamanio ya kisiasa usipoangaliwa kwa makini na kwa busara, hugeuka kuwa maangamizi kwa umma.
CWT na walimu walipaswa kuwa makini katika kubuni namna ya kushinikiza madai yao, ili yafanyiwe kazi huku wakikumbuka kuwa, wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakijenga mazingira na kutoa kauli zinazolenga kulifanya taifa lisitawalike na kudumbukia katika vurugu. Je, mgomo na mgogoro huu uliowahusisha wanafunzi wadogo kuandamana, kuvuja vioo vya magari kwa kuyapiga mawe, kufunga barabara na kuharibu mali za umma na za watu binafsi ni sehemu ya mchakato huo wa kuivuruga nchi isitawalike? Je, nani anapaswa kuwajibika kisheria kwa usumbufu na uharibifu huo wa mali?
Kwa jumla, si tabia ya Watanzania walio wazalendo kutumia ubabe au njia za kikatili kuwasilisha maoni au malalamiko. Tabia hizo zina wenyewe na wanajulikana, je na wao walishiriki katika kuandaa mgomo huo ndiyo maana viashiria vya tabia zao zimeonekana katika yatokanayo na mgomo huo?
Huu ndio wito wangu kwa viongozi wa Serikali hasa Jeshi la Polisi kwamba, watu wameyachoka maandamano na vurugu, je mnasubiri nini kuwafikisha mahakamani wanaotumia uhuru wao kuvunja sheria kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni, maoni gani yanatolewa kwa kuvunja sheria tena za watoto?
Watanzania watafarijika kuona CWT imewafidia wanafunzi wote waliathirika kwa namna moja ama nyingine, pia umma utafurahi kama wachochezi wa suala hili watafikishwa mahakamani, kwa tuhuma za uchochezi na ukatili kwa watoto.
MUNGU IBARIKI TANZANIA.