Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Siri ya mauaji ya Zanzibar yafichuka

Print PDF

*Mkono wake unahusisha taasisi za kimataifa
*Rai lanasa CD ya video ya kulipa kisasi, kuua
*Orodha ya maaskofu wanaosakwa yabainika
TAASISI ya kimataifa ya kidini kwa kushirikiana na makundi mawili ya kigaidi ya nje ya Tanzania yanatajwa kuhusishwa katika matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa kiimani Zanzibar, gazeti la Rai limebaini.


Mbali ya taasisi hizo ambazo tayari uhusiano wake wa kikazi na makundi ya Al Shabaab na Boko Haram umeshaanza kuchunguzwa, matukio hayo ya mauaji yanahusishwa pia na kauli zinazoonekana kuwa za kichochezi zinazotolewa na Sheikh mmoja anayeishi nchini mwenye asili ya Kongo (jina tunalo)

Utafiti uliofanywa na gazeti la Rai umebaini kwamba, mikakati inayohusisha kutekelezwa kwa mauaji hayo na vitendo vingine vya kujeruhi na kuchoma makanisa inahusisha pia vikao vya siri ambavyo kimojawapo kilipata kukaa nchini Nigeria na kujumuisha viongozi wa kundi maarufu nchini humo la Boko Haram.

Vyanzo kadhaa vya habari vilivyozungumza na Rai, vinaeleza kwamba, matukio hayo ya kupangwa yana malengo kadhaa yakiwamo kulazimisha muungano kuvunjwa na kulipiza kisasi dhidi ya matukio ambayo yamepata kutokea nje ya Tanzania.

Hata hivyo, gazeti hili la Rai halikuweza kuthibitisha sababu ambazo zilisababisha kisiwa cha Unguja chenye waumini wengi wa Kiislamu kuwa mlengwa nambari moja wa mikakati hiyo ya kihalifu ambayo tayari imelaaniwa na viongozi na waumini wa Kikristo na Kiislamu.

Habari zaidi za uchunguzi zinaeleza kwamba, wauaji wanaotekeleza mauaji hao na mipango ya namna hiyo ya kihalifu ambayo tayari imesababisha vifo vya mapadri wawili wa Kanisa Katoliki wanatumia njia ya maji kutoroka na kwenda nchi jirani baada ya kufanikisha uhalifu huo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, vijana wa Kizanzibari wanaopanga na kuendesha mauaji hayo wanaelezwa kupata mafunzo mahusisi ya kutumia silaha na kulenga shabaha kutoka nchini Somalia liliko kundi la Al- Shabaab.

Mbali ya hayo, CD ya video ambayo RAI imeiona na inayodaiwa kusambazwa kwa siri kwa watu mahususi inamuonyesha sheikh mmoja anayetajwa kwa jina moja tu la Kapungu akiwahamasisha Waislamu kujihami na kulipa kisasi.

Katika sehemu moja ya kanda hiyo, sheikh huyo ambaye uraia wake unatajwa kuwa ni wa kutoka nchi moja jirani, anasikika akiwataka Waislamu kutokubali kuliacha tukio la sheikh mmoja wa Mombassa kuuawa likapita pasipo kujibiwa.

Sheikh wa Mombassa anayetolewa mfano ni Aboud Rogo ambaye anadai aliuawa ndani ya gari lake, yeye, mkewe na baba yake mzazi.

“Tulipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba Sheikh Aboud Rogo Mwanaharakati maarufu wa Mombassa, amepigwa risasi ndani ya gari yake, akiwa na familia yake akielekea Nairobi.

“Yeye kapigwa risasi nyingi sana mwilini, mke wake pia na baba yake mzazi kapigwa risasi. Yeye na familia yake wamekufa, aliyenusurika ni mtoto mdogo aliyekuwa naye ndani ya gari yake. Ziko kauli zinasema kwamba amepigwa risasi 16 mwilini, ziko kauli zinasema kapigwa risasi 22.

“Mpigaji alitaka kuhakikisha haponi, na kweli Aboud Rogo alikufa papo hapo. Vyombo vyote vya habari ambavyo vingi ni vya makafiri, vilianza kutangaza Sheikh Aboud Rogo ameuawa na watu wasiojulikana.

“Waislamu wa Mombasa hawakusaka, trafiki waje, hawakutaka polisi wachunguze, polisi wa kwanza aliyefika, hakuweza kukaa pale, ndani ya saa tatu, Waislamu walimzika Sheikh Aboud Rogo.

“Waislamu wa Mombasa walikuwa hawana haja ya polisi kuchunguza kwa sababu wao wanaposema kauawa na watu wasiojulikana, Waislamu wana hakika kauawa na watu wanaojulikana. Waislamu walisema kauawa, hatuna haja.

“Baada ya hapo kukatokea fujo Mombasa magari kuchomwa moto na kuharibiwa, mimi nikiwauliza jamaa zangu Mombasa hali inaendeleaje wanasema hatujatoka ndani siku ya pili sasa. Shughuli zimesimama kwenye mji wa Mombassa.

“Niliwakumbusha Waislamu wa Mombasa warudi kwenye Kuraan, inasema akiuawa Sheikh Aboud Rogo au yeyote, unavunja magari ya watu? Kuraani inasema mlipe kisasi, akiuawa mwislamu huvunji gari ya mtu, unalipa kisasi, jicho kwa jicho, meno kwa meno.

“Kauawa Aboud Rogo, tafuta Askofu mmoja naye muueni, tafuta Kardinali na wewe muue, kauawa mwislamu tafuta padre muue tafuta mchungaji muue, wataacha hawa. Mkiua wanne watashika adabu.

“Kama hamna uwezo huo jipangeni jiratibuni, naanza fikra ngumu. Tafuta kardinali muue kwa kificho au kwa dhahiri,” anasikika akisema sheikh huyo katika mhadhara huo.

Vitisho dhidi ya viongozi wa dini nchini
Wakati CD hiyo ikisambaa, uchunguzi wa RAI unaonyesha kwamba, vitisho dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo wakiwamo, Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augustine Shao, Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa vikabainika.

Mbali ya hao, maaskofu wengine ambao waliwekwa katika orodha hiyo baada ya majina yao kutajwa kwa njia ya vipeperushi ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Valentine Mokiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.

Katika orodha hiyo na kwa sababu ambazo bado hazijawekwa hadharani lilitajwa pia jina la Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Mussa Soraga ambaye hivi karibuni alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana mjini Unguja.

Kauli za Maaskofu
Baada ya taarifa kufika ndani ya chumba chetu cha habari kwamba zipo taarifa za viongozi kadhaa kuuawa, tuliwatafuta wahusika wakuu na katika mahojiano nao walikuwa mawazo mbalimbali huku wakikemea vitendo vya aina hiyo.

DK. Valentine Mokiwa:
“Pengine sasa unaongea na marehemu mtarajiwa. Tunatamani sana kukutana na vyombo vya usalama, lakini fursa zilizopo ni ndogo, twende wapi sasa, tukinyamaza tutakufa, tusiponyamaza tutakufa, wakitaka watulinde, wasipoamua wasitulinde, lakini hatuna cha kupoteza,” alisema Askofu Mokiwa.

Dk. Mokiwa alilieleza RAI kwamba, Sheikh Kapungu alitakiwa kuwa wa kwanza kuvisaidia vyombo vya ulinzi nchini juu ya matukio ya mauaji ya viongozi wa dini ya Kikristo yanayoendelea Zanzibar akisisitiza kila alichozungumza katika CD ambayo naye alikiri kuiona ndicho kinachotokea sasa.

“Huyu angekuwa ndio wa kwanza kuhojiwa. Iweje hasira ya tukio la nchi jirani ije Tanzania na yote aliyoyazungumza ndio yameanza kutokea.

“Wakristo sasa angalieni mnachokula, angalieni mapito yenu….hamko salama, lakini kanisa halijamtangaza mtu kuwa adui yake, lindeni wenyewe nyumba zenu za ibada na tusikubali alinde mtu mwingine, sababu hakuna ulinzi, hatulindwi. Kila kichwa cha Mkristo hakipo salama sasa, Mungu alijaalie kanisa katika nchi hii, halitaondolewa na halitafutwa,” alisema Dk. Mokiwa.

Askofu Michael Hafidh:
Katika mahojiano na RAI, Askofu Hafidh anasema; “sasa sio wakati tena wa maombi peke yake. Tunasema tumechoka, haya yanayotokea Zanzibar yamepangwa,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Askofu Hafidh anasema mara baada ya kupata taarifa za vitisho vya kuuawa kwa viongozi wa dini ya Kikristo Zanzibar alipeleka taarifa hizo kwa jeshi la Polisi Zanzibar, hata hivyo hakupata ushirikiano.

“Nimezungumza uso kwa uso na Kamishna wa polisi Zanzibar na kumpatia CD hiyo, lakini hakuna alichofanya, nikamweleza asipochukua hatua lazima litatokea jambo kubwa.

“Siogopi najua siku moja nitakufa, nasema wazi sina imani na mfumo mzima wa usalama wa Taifa na jeshi la polisi Zanzibar, wahalifu wamo ndani ya jeshi la polisi.

“Wakristo wa Zanzibar bado tunayo imani kubwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Nchimbi, lakini si kwa sababu yeye ni mkristo mwenzetu, ni kutokana na uwezo wake wa kufuatilia mambo, lakini anaangushwa na polisi Zanzibar,” anasema Askofu Hafidh:

Kardinali Pengo:
“Tukio hili lingeweza kuzuilika, lakini uzembe uliofanywa na vyombo vya usalama kwa kushindwa kufuatilia taarifa zilizofikishwa kwao kupitia, CD na vipeperushi mbalimbali, hasa hasa mara baada ya tukio la siku ya Krismasi la kupigwa risasi, father Ambrose Mkenda,”

“Hili si tukio la dharura, kiasi kwamba watu wetu wa usalama wa Taifa washindwe kuzuia, hili lilijulikana na lingeweza kuzuilika,” anasema Pengo katika mahojiano na RAI.

Askofu Augustine Shao:
“Mara baada tukio la kushambuliwa padri Ambrose na Sheikh Soraga, tulipata ujumbe ukisema, tumewaweza na bado tunaendelea, tunao vijana wa kazi wenye mafunzo waliyoyapata Somalia,” alisema Askofu Shao.

Askofu Shao anasema licha ya kufikisha ujumbe mbalimbali za vitisho kwa jeshi la polisi na uongozi wa juu Ikulu Zanzibar, hakuna kilichofanyika, badala yake walionekana wanataka kueneza chuki za kidini Zanzibar.

“Haturidhishwi na utendaji kazi wa mfumo mzima wa usalama wa taifa na jeshi la polisi Zanzibar kupitia kwa kamishna wake, Mussa Alli Mussa,” alisema Askofu Shao.

Jeshi la Polisi Zanzibar:
Akizungumza na RAI, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa alisema ingawa lawama nyingi zinaelekezwa kwa Jeshi la Polisi, anawalaumu wananchi waishio kwenye eneo alilouawa Padri Evarist Mushi kwamba walifanya uzembe kuchelewa kutoa taarifa za kuwapo watu wasiowafahamu katika eneo lao.

“Unaweza kusikia mengi kwa sasa, lakini licha ya kuwapo vipeperushi vinavyotishia maisha ya viongozi wa dini, wananchi nao wana nafasi yao ya ulinzi miongoni mwao.

“Kwa mfano wauaji wa Padre Mushi walionekana na wananchi wa eneo hilo tangu saa 11 alfajiri wakipitapita, lakini wananchi hawakuwatilia wasiwasi, mpaka tukio lilipotokea,” alisema Kamishna Mussa.

Akizungumzia tuhuma za viongozi wa dini ya Kikristo kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa alisema, baada ya kupokea malalamiko ya viongozi wa dini juu ya tishio la kuuawa, walifuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kupekua nyumba za watuhumiwa lakini hawakupata ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Kamishna Mussa pia alisema yeye alikuwa hajapata taarifa za kuwapo kwa CD inayohamasisha kuuawa kwa viongozi wa dini ya Kikristo na kusema yeyote aliye na CD hiyo anaweza kuwasilisha polisi.

Kamishna Mussa alisema polisi inaendelea kufanya uchunguzi kubaini iwapo kweli matukio hayo yanahusishwa na ugaidi na kufadhiliwa na baadhi ya jumuiya za nchi za Kiislamu.

“Bado sisi tunasema huu ni uhalifu, Inaweza ikawa ugaidi lakini bado Jeshi la Polisi Zanzibar hatujafikia hatua ya kutoa kauli ya mwisho kuyahusisha matukio ya Zanzibar na ugaidi…ngoja tumalize upelelezi wetu nadhani tutafika pazuri na kutangaza kuwa hili ni tukio la kigaidi, au la,” alisema Kamishna Mussa.

Polisi Makao Makuu
Kama ilivyokuwa kwa Kamishna Mussa, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ASP Advera Senso naye aliliambia RAI kuwa alikuwa hajapata kuiona au kuisikia CD inayotoa wito wa kuuawa kwa viongozi wa kidini.

“Hatuna taarifa hizo za kuuawa kwa viongozi hao, wamekwambia wewe?, Hebu njoo ofisini tuzungumze kwa undani juu ya hili,” alisema ASP Senso.

 

Maoni  

 
0 #10 KISOGO DOGO 2013-05-14 07:29
Huwezi kuchukuwa matukio makubwa kama haya ukayashabihisha na maneno ya mtu ambae ambapo luga kama hizo tumezoea kuzisikia nchini petu kupitia CDs tofauti tokea miaka ya 1980 na mengine yalikuwa makali kuliko yaliyoongelewa kipindi hiki. Kisha huwezi kutuambia kuna CD zinazotolewa kwa siri zinazoonesha dhamira hizo mbaya, hiyo ni mihadhara iliyokwisha zoeleka ambapo kwenye dini hiyo ipo wazi na hakuna kiongozi anaeficha katika kuitafasiri dini/quran inaongea nini kwenye kutenda na kupatikana kwa haki, yeye ananukuu tu. Kuna mengi ya kuiachia serikali iweze kufanya kazi zake kiuadilifu zaidi, kuna uwwezekano mkubwa kwamba kuna maadui wa Uchumi wetu wanaoweza kutumia mifumo ya dini kutupiganisha, lakini kwa kuwa tunasubiri ni jina gani tu litaappear kwenye tuhuma tuseme ni tukio la kidini basi hii dhana itaipeleka nchi pabaya sana.
Nukuu
 
 
+1 #9 abdo 2013-05-03 16:15
Huyu mwandishi maalumu kafanya kazi kubwa ya kuyapanga mambo ambayo hayajengi udugu baina ya Watanzania bali yanachangia mfarakano.Mauaj i ya raia wa dini yeyote lazima yalaaniwe na hatuwa za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mhalifu au wahalifu.Kwa mtazamo wa taarifa hii,inaonekana kwamba mpango wa makusudi wa kuichafua Zanzibar umo katika matayarisho kama vile tulivoona matokeo katika nchi kama Iraq.Na hii si ajabu hasa baada ya kuhusishwa kwa wapelelezi wa kigeni katika tukio ambalo mpaka sasa mahakana haijatoa uwamuzi wake.kUHUSU BWANA JULIAS,naona UDINI NA UKABILA umeuweka mbele badala ya UWANANCHI.La kushangaza ni jazba kubwa inayoonekana baada kifo cha askofu mmoja huko Unguja,LAKINI inasikitisha hatukuona jazba kama hizi walipouliwa wananchi wa PEMBA katika mwaka wa 2001 kwa kutungwa risasi toka nchi kavu hadi angani.Tuwache lugha za uchochezi na badala yake tulete lugha za uwiano mwema
Nukuu
 
 
0 #8 JULIUS 2013-02-27 15:11
Hakika liliosemwa na babu ni kweli, Kilichopo kisogoni mwako haulioni! Tanzania tu kitukimoja tena kwa maridhiano kwa moyo mweupeeeeeeeeee ee! Nilitegemea anaezungumuzia muungano atoe yale aonayo mapungufu yake ili yafanyiwe kazi na si kuchochea kuuvunja, naimani hawajui umuhimu wake na wasipewe hata mwanya hata kidogo, waonekanapo waadhibiwe kama paka aliekunywa chakula cha mtoto! na vile vile waislamu wasijisahau kiasi wadhani hii nchi yao, hi ni nchi ya watanzania wenye dini mbalimbali, rais kuwa mhislamu au mkiristu sio nchi kuwa kama dini yake. nasema hivi maana tangu mheshimiwa aingie madarakani ndugu zangu kidogo wamejisahau kuwa hapa uarabuni,
Nukuu
 
 
0 #7 Ntandu 2013-02-26 12:04
Binafi nimeuona uchochezi huu kupitia You Tube, kweli inasikitisha sana kuona watu wakijinasibu kwa mambo ya aibu namna hii. Hawa si waislamu halisi bali ni kundi fulani la wahuni wenye malengo yao machafu juu ya Zanzibar na Tanzania. Waumini wa kweli wa Uislamu wanaamini kuwa dini yao ni dini ya Amani. Ikiwa hawa (wahusika wa mauaji)wanahisi Amani iliyopo inachafuliwa, haya yanayofanyika ndio njia sahihi ya kuirejesha Amani?
Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama inaonekana iko likizo. Haiwezekani maefu ya wananchi wa kawaida kupata taarifa za mipango ya kutisha ya mauaji (ipo kwenye mitandao ya kijamii) na vyombo vya usalama vikadai havina taarifa hizi. Hii inaonyesha aidha kuna uzembe wa makusudi au wanakaa maofisini wakisubiri kuletewa taarifa na wananchi. Kwa mtindo huu tutarajie maangamizi makubwa ambayo hata wao pia hayatawakwepa.
Nukuu
 
 
0 #6 Mohamed 2013-02-26 06:07
habari hii mimi nasema ni ya uongo na uzushi mtupu nasema hivyo kwa sababu mbili ( 2 ) kwubwa.
1. habari hii imeandikwa na muandishi ambae hajajieleza jina lake .
2. inaonesha dhahiri huyu muandishi wa habari hii ana chuki na uislamu na waislam. sisi wazanzibari tunaishi vizuri na ndugu zetu wakristo kwa kuthibitisha haya mimi binafsi nimeowa na mke wangu wazazi wake woto ni wakristo , sasa kama kuna chuki kati yetu wangekubali kuniozesha mtoto wao? sisi wazanzibari tuna msemo tunasema hivi kila mtafuta janga basi hula na ............... ............... AHSANTE
Nukuu
 
 
0 #5 Ndewinyi 2013-02-25 08:55
Ni vyema Serikali ikaamka usingizini na kukabiliana na tishio hili. Mbona hatumsikii Rais akitoa kauli? Tunasikia tu Waziri kasema hivi, Mkuu wa mkoa/wilaya kasema hivi, Katibu Mwenezi wa Chama fulani kasema hivi n.k. Rais atekeleze wajibu wake wa Kikatiba wa kuhakikisha usalama wa raia, uhuru wa kuabudu na haki ya kuishi. Vinginevyo anaweza kufikiriwa kuwa anaunga mkono ugaidi huu kichinichini. Asilichukulie suala hili kimzaha. Iko siku tutamwajibisha yeye na Waziri Mkuu wake kwa kushindwa kuitetea Katiba kama walivyoapa kwenye viapo vyao. Shime wananchi tutetee amani ya nchi yetu. Viongozi wa kisiasa na Jeshi la Polisi Zanzibar wamulikwe. Wana ajenda ya siri. Wanavyofuatilia ugaidi huu inatia shaka kubwa.
Nukuu
 
 
0 #4 olupesenge 2013-02-23 10:52
Haya ni matunda aliyoyapanda kikwete katika safari yake ya kuelekea ikulu,sasa ndo tunayavuna.Na wakristu acheni kuilaumu serikali,nyie ndo mulitwambia huyu mtu ni chaguo la Mungu.Acheni kuwa wapole hii ni vita dhidi yenu ipo mlangoni,tokeni na pambaneni,la sivyo mtakwisha.
Nukuu
 
 
0 #3 master wa tanzania 2013-02-22 14:17
jaman uongozi usipoangalia kwa makini suala hili na kulizuia tutajikuta tukiingia ktk vita visivyo na maana,ushauri serikari ifuatilie kikamilifu bila ubagudhi wa kidini.
Nukuu
 
 
0 #2 OMWANA WATANZANIA 2013-02-21 14:40
Jamani hizi CD za "Kongamano la Mfumo Kristo Kisiwani Pemba 2/10/2011", n.k mmepata kuziona. Zitazameni! Je huyu mwendesha makongamano haya ana malengo gani kwa taifa hili? Ukitazama CD hizi utajua Makusudi ya kikundi cha uamsho Zanzibar ni nini? Kwa nini Uamsho wanataka Muungano uvunjwe? n.k. Mwisho serikali ishughulikie mizizi ya uhasama wa kidini bila woga wala kigugumizi, viginevyo taifa hili limeanza na linatumbukia kwa uhakika ktk vita vya kidini.
Nukuu
 
 
+1 #1 OMWANA WATANZANIA 2013-02-21 14:40
Jamani hizi CD za "Kongamano la Mfumo Kristo Kisiwani Pemba 2/10/2011", n.k mmepata kuziona. Zitazameni! Je huyu mwendesha makongamano haya ana malengo gani kwa taifa hili? Ukitazama CD hizi utajua Makusudi ya kikundi cha uamsho Zanzibar ni nini? Kwa nini Uamsho wanataka Muungano uvunjwe? n.k. Mwisho serikali ishughulikie mizizi ya uhasama wa kidini bila woga wala kigugumizi, viginevyo taifa hili limeanza na linatumbukia kwa uhakika ktk vita vya kidini.
Nukuu
 

Toa Maoni


Waliotutembelea