SEKTA ya Elimu Tanzania imeendelea kuwa na mgogoro kwa miaka mingi, jambo linalosababisha elimu kushuka kwa kiwango cha kutisha. Uchunguzi uliofanywa na RAI, umebaini kuwa, moja ya sababu inayochangia wanafunzi kutojua kusoma na kuandika, ni migogoro ya walimu kugoma mara kwa mara, jambo ambalo linawakatisha tamaa walimu wenye moyo na kufanya kazi.
Mwandishi wa RAI alizungumza na baadhi ya walimu katika Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, aakiwamo Mwalimu Abdi Selemani, wa Shule ya Sekondari Kasangezi. Alisema kuwa walimu wengi wamekwisha kata tamaa, tangu zamani, kutokana na kuvunjwa moyo na Serikali.
Alisema kwamba walimu wamekuwa ni watu wa tabaka la chini, hata kudharaulika katika jamii, tofauti na zamani ambapo walimu walikuwa ni watu wanaoheshimika kwa taaluma yao.
“Tumekuwa watu wa kudharauliwa na haya yote ni sababu ya Serikali kututupa na kutufanya kuwa watu wa tabaka la chini, jambo ambalo si kweli mkumbuke kuwa sisi walimu ndio tunaowatoa viongozi bora na sisi walimu ndio tunaoifanya nchi kuwa na wataalamu wa fani mbalimbali.’ Alisema.
Mwalimu Selemani, alisema kila siku walimu wamekuwa ni watu wa kuhangaika na maisha magumu, hata mara moja hawajawahi kufikiriwa angalau waongezewe posho ya mazingira magumu, lakini pia walimu hawana pesa za malipo ya muda wa ziada, japo kwa muda wote walimu wanakuwa wapo kazini—hasa katika shule za bweni.
“Inafikia kipindi mwalimu mwenye shahada, anapata mshahara mdogo kuliko katibu mahsusi wa Afisa Elimu kwa sababu mwalimu hana fedha za malipo ya ziada tofauti na sekta nyingine.”
Aliiomba Serikali isiwagawe katika matabaka wafanyakazi wake kwa kuwa jambo hilo, litawafanya walimu wengi kufundisha pasipokuwa na moyo wa ualimu.
“Kumekuwa na dhana potofu kuwa ualimu ni kazi ya watu walioshindwa kabisa watu wa daraja la chini na ambao wamekosa mahali pa kwenda hii inawafanya hata walimu wenyewe kufundisha bila kuwa na wito kutoka ndani.”
“Tunaiomba Serikali kupanga ngazi za mishahara kuendana na kiwango cha elimu ya mtu. Kwa mfano, daktari mwenye shahada, alipwe sawa na mwalimu mwenye shahada, kadhalika na viwango vingine vya elimu.”
Alisema kwa kufanya hivyo, itasaidia kupata mwalimu wa kweli ambaye hatakimbia ualimu kutokana na maslahi madogo.
“Wazazi wengi wamekuwa hawataki watoto wao wapewe adhabu wanapofanya makosa na hasa watoto wa kike. Usishangae ukazuliwa jambo ambalo hukulitegemea kutoka kwa mzazi. Sasa kutokana na maslahi mabovu na wakati huo mnasumbuliwa na wazazi, walimu wengi wanawaacha wanafunzi watakavyo.”
Abdi alisema walimu wamekuwa na wakati mgumu, hasa wazazi wanaposhindwa kuwapa ushirikiano walimu—hasa wanaposhuka kitaaluma.
Alisema mgomo ni kama ulishaanza zamani kutokana na walimu kukata tamaa kwa sababu Serikali haitaki kusikia maombi yao na kuyatekeleza, hivyo walimu wengi wapo tu na wanafundisha bila kuwa na moyo wa kazi.
“Mbona mgomo kwa walimu ulishaanza zamani sana, jamani kwani mnadhani mgomo ni huu mnaouona sasa? Ili kujua kama walimu walishagoma toka zamani ndio maana tunashuhudia mwanafunzi mpaka anafika Darasa la Saba, hajui kusoma wala kuandika. Hayo ni matokeo ya mgomo ulioanza muda mrefu.”
Alisema Serikali isitafute mchawi kwa kuendelea kuwafanyia vitisho viongozi wa Chama cha Walimu, kwani mchawi wa migomo hiyo ni Serikali yenyewe kwa kuendesha kimabavu na kutosikia mahitaji ya walimu.
Aidha wazazi wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa walimu hasa wanafunzi wanapokuwa si watiifu darasani, jambo hilo huwavunja moyo walimu na kuwaacha wanafunzi kujiendesha kadri watakavyo.
Venance Balampama, ni mfanyabiashara wilayani Kasulu, alisema kuwa mfumo wa elimu wa sasa, unachangia kushuka kwa kiwango cha elimu kutokana na kwanza, wanafunzi hawatakiwi kurudia darasa hata kama hawajui kusoma na kuandika Tofauti na zamani ambapo mwanafunzi asingeweza kupanda darasa, kama hajui kusoma na kuandika.
Pia alisema walimu wanazuiliwa kuwachapa viboko wanafunzi, kitu hicho kwa maoni yake, kinashusha kiwango cha heshima na kitendo hicho kinasababisha walimu kukata tamaa ya kuwaadabisha watoto.
“Sisi zamani tulikuwa tunapata viboko kweli na kwa njia hiyo tuliweza kusoma kwa bidii, wakati mwingine kwa kuogopa kuchapwa na ndio maana mpaka leo mnatuona hivi, lakini Serikali yetu kwa kufuata matakwa ya wafadhili, wamekuwa hawataki wanafunzi kuchapwa na hata wazazi wameingiwa na mdudu huyo.
“Wanafunzi wa kiume wamekuwa wakiwakunjia ngumi walimu wao na wazazi wanakubaliana na watoto wao, hivyo kwa mazingira kama hayo, tutarajie kushuka kwa kiwango cha elimu, kwani walimu hawatafundisha kwa moyo kama walimu wa zamani.”
Alisema mwalimu anakuwa na mazingira magumu katika kazi yake—hasa ikizingatiwa kwamba maisha wanayoishi ni magumu—anaona ni bora amuache mwanafunzi afanye atakavyo, jambo ambalo linaendelea kudidimiza nidhamu na kusababisha kushuka kwa kiwango cha elimu.
Aidha aliiomba Serikali kurekebisha baadhi ya sera na sheria ambazo wamezianzisha hivi karibuni, kwani zinashusha kiwango cha elimu na heshima kwa wanafunzi wenyewe mbele ya jamii.
Balampama anasema katika miaka ya nyuma, mzazi yeyote kumuadhibu mtoto anapofanya kosa, ilikuwa ni jambo la kawaida na hii ilisaidia katika kuendeleza nidhamu katika jamii, tofauti na sasa ambapo wazazi wamekuwa chanzo cha uharibifu wa tabia kutokana na wazazi kuwalea watoto wao bila maadili.
“Siku hizi ikitokea ukamkuta mtoto anafanya makosa yanayostahili kuadhibiwa na ukamuadhibu mtoto wa mtu, utarajie kufuatwa na mama wa mtoto mwenye hasira, huku akiwa kashikilia kanga mkononi na haishangazi kama ugomvi utazuka kutokana na mzazi fulani kumuadhibu mtoto wa jirani.”
Alisema hali hiyo pia husababisha kushuka kwa kiwango cha elimu kutokana na walimu kuogopa kupigwa, hasa na wanafunzi ambao ni wakubwa.
Mwalimu Michael Kazembe, ni Mkuu wa Taaluma, Shule ya Sekondari Kinkati iliyopo wilayani Kasulu. Yeye anasema uhaba wa miundombinu shuleni, ni sababu kubwa inayosababisha walimu kukata tamaa.
Aidha anasema walimu wamekuwa wakionewa na kuonekana kuwa ni watu wa shida, hivyo kuwafanyia wanavyotaka na kusahau kuwa wataalamu na matabibu, wote msingi wao ulikuwa katika elimu ya msingi na sekondari.
Anasema hivi sasa Serikali ni kama inaandaa bomu ambalo likija kulipuka wa kulizima hata kuwepo kutokana na kwamba kwa sasa Sekta ya Elimu imetelekezwa na Serikali na kuonekana kama haina maana sana.
“Taifa lisilokuwa na wasomi na wavumbuzi ni taifa ambalo linaekea kufa, hivyo Serikali inaendelea kuzembea sekta hii, inaendelea kujichimbia kaburi.”
Alisema kwa sasa elimu inaendeshwa hovyo hovyo na kwa hiyo, Tanzania itarajie wataalamu wa hovyo hovyo hapo baadaye, kwani ndicho ambacho kitakuwa kimepandwa na wataalamu.
Alisema bado pia kuna tabaka kati ya walimu na wanafunzi walioko vijijini na wa mijini—mazingira ya walimu vijijini ni mabovu—yameendelea kuwa mwiba kwa wanafunzi na walimu. Aidha, vifaa navyo vimekuwa tatizo hasa vya maabara.
“Shule nyingi hakuna maabara kama shule hii ya Kinkati hakuna maabara, lakini pia kuna mwalimu mmoja tu wa sayansi kwa shule nzima. Hapo unategemea nini? Mwalimu mmoja ataweza kumudu kufundisha madarasa manne, peke yake, tena bila kuwapo maabara? Aliuliza Kazembe.
Aliiomba Serikali kuhakikisha inawachukulia walimu kama daraja muhimu ili kuwawezesha kupata walimu bora, ni lazima wajipange katika kuchagua wasomi, waliopata alama za juu na kuwaboreshea maisha walimu ili waweze kuwafundisha wanafunzi kwa moyo.
Aidha, ameiomba Serikali kuboresha miundombinu na kuzingatia umbali wa wanafunzi na walimu wanapotoka na sehemu shule zilipo.
Maoni
serikali ianze utaratibu wa kuwapanga walimu wa sayansi wenye diploma ili waboreshe elimu ya msingi kwani walimu wa shahada wapngew sekondari kwani kwa sasa wanahitimu wengi.