*Viongozi waandamizi watumia mali za Serikali na taaluma zao kwa maslahi binafsi
*Walinzi nao washirikiana na wafanyakazi kula “dili” za nje
Ufisadi na matumizi mabaya ofisi za umma unaendelea kuzitafuna taasisi za Serikali na idara zake, safari hii ikiwa ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Rai limegundua
Gazeti hili limegundua kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Wizara hiyo wamegeuza ofisi za serikali kufanya biashara badala ya umma na makampuni binafsi ya kuchimba visima vya maji ambavyo ni kinyume na sheria ya utumishi wa umma.
Gazeti hili limegundua kuna mtandao mrefu ukihusisha pia baadhi ya walinzi wa ofisi wa Wizara hiyo makao makuu Ubungo Dares salaam.
Kama na mteja inakubidi kwanza utoe maelezo pale getini kwa walinzi nini hasa unakitaka kama ni “dili” watakuambia cha kufanya na watakuletea mtu wakufanyia shughuli hiyo nje ya ofisi za serikali.
Orodha ni ndefu. Gazeti hili limepata nyaraka ambazo zinaonesha jinsi baadhi ya maofisa wa Wizara hiyo wanavyofanya biashara kwa kutumia mihuri na vifaa vingine vya Serikali kujiingizia mapato.
Miongoni mwa watu wanaofanya biashara hii ni John Bulugu ambaye anajitambulisha Fundi wa Kuchimba visima (Principal Drilling Technician) kama kuna dili wakati yeye cheo chake ni Fundi umeme wa Wizara hiyo (PT-EI).
Nyaraka zinaonesha kuwa Bulugu alitoa na kusaini mchanganuo wa gharama (quotation) za kuchimba visima wa thamani ya shilingi milioni 17,800,000 kama mtaalam wa visima wa Wizara tarehe 9/7/2012 kwa kampuni moja ya jijini Dar es salaam kama kampuni husika ingetoa kazi kwa serikali.
Lakini wakiwa katika mazungumzo Bulugu aliwaeleza wateja wake kama wanaona gharama za serikali ni kubwa basi ange watengenezea mchanganuo mwingine kwa kutumia kampuni binafsi(jina tunalihifadhi)
Baada ya mazungumzo walikubaliana na Bwana Bulugu na aliwapatia mchanganuo mwingine wa gharama ya shilingi milioni 13,064,000/= ikiwa pungufu ya shilingi milioni 4, 736,000/=kwa kutumia kampuni binafsi huku akijitambulisha na kusaini kama Fundi wa kuchimba visima (Principal Drilling Technician) siku hiyo hiyo tarehe 9/7/2012
Aidha katika uchunguzi wa gazeti hili unaonesha kwamba hata kampuni aliyotumia kujipatia hela haifanyi kazi kutokana na wakurugenzi wake kufariki dunia katika nyakati tofauti tangu mwaka 2002.
Walipotafutwa viongozi wa utawala Wizara ya Maji na umwagiliaji, kiongozi mmoja ambaye alitaka jina lake lisitajwe gazetini, alimwambia mwandishi kwamba kweli Bulugu ni rafiki yake na ni mtu wa umeme siyo maji, lakini akataka aonane na Bulugu ili haya mambo yasiandikwe gazetini .
Alipotafutwa Bwana Bulugu kwa njia ya simu ili adhibitishe alimwambia mwandishi kwamba ana kazi nje ya ofisi na si vizuri akazungumza kwa simu akaahidi kuonana na mwandishi nje ya ofisi.
Lakini kila alipotafutwa na mwandishi kwa karibu wiki nzima, Bulugu alimwambia mwandishi; ngoja akae sawa atamtafuta. Juhudi za kumtafuta Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Maghembe zilishindikana baada ya mwandishi kuambiwa kuwa Waziri yuko Dodo kwenye vikao vya Bunge.