Mbunge: Kuna unafiki CCM

Print

*Yadaiwa kuwa atashitakiwa kwa Kikwete, Kinana
*Adai kuwa hiyo ni sumu hatari ndani ya chama hicho

MBUNGE wa Jimbo la Mwibala (CCM), Kangi Lugola, amesema tuhuma dhidi yake kuwa anakidhoofisha chama chake bungeni hazina msingi wowote, na kamwe haziwezi kumtisha.

Lugola alitoa kauli hiyo katika mahojiano na Rai Jumanne wiki hii, baada ya kuwapo taarifa za yeye na wabunge wengine wawili kushitakiwa kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na mwenendo wao wa kuikosoa Serikali bungeni.

Mbali ya kuwapo taarifa za wabunge hao kushitakiwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, taarifa nyingine zimedai kuna mkakati mkubwa wa kuwashughulikia katika kikao kinachotarajiwa kufanyika wiki chache zijazo kati ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na wabunge wa chama hicho mjini Dodoma.
Mbali ya Lugola, wabunge wengine wanaonyoshewa vidole ni Deo Filikunjombe wa Jimbo la Ludewa na Luaga Mpina wa Jimbo la Kisesa.

Akizungumza kwa kujiamini, Lugola alisema; “Kuna wabunge wa CCM wenye dhana potofu kabisa, wao wanadhani au kufikiri kuwa Mbunge anayetokana na chama chetu hapaswi kuhoji Serikali yake suala lolote linalohusiana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

“Dhana hii potufu inaambatana na woga na unafiki, ndio sababu wale ambao tunaikosoa Serikali kwenye mambo ya msingi kwa lengo la kuisaidia na wakati huo huo kuimarisha chama, tunaonekana tatizo.

“Dhana hii inapandikiza sumu hatari miongoni mwa viongozi na wanachama, na matokeo ya sumu hii mbaya ni kuzaa chuki na fitina, jambo ambalo ndilo linalotokea sasa miongoni mwa wabunge.

“Hali hii ikiachiwa bila kukomeshwa kwa vitendo na si maneno, chama kitadumaa, kitakuwa legelege na matokeo yake ni kuzaa au kuwa na Serikalu legelege.

“Ndio maana kuna wabunge wenye fikra chanya ambao hawataki Chama Cha Mapinduzi kifike huko, matokeo yake ni msuguano unaoonekana sasa.

“Hizi habari za kushitakiwa kwa uongozi wa juu wa chama hazininyimi usingizi kwa sababu ni maoni ya mtu, watu au wabunge wanafiki wenye ajenda zao binafsi.

“Siamini kama CCM ninayoifahamu na inayofahamika kwa Watanzania inaweza kukaa chini kujadili na hatimaye kukubaliana na wabunge wanafiki.

“Serikali au chama bila kukosolewa kitabweteka, kwa mimi na baadhi ya wabunge wenzangu ambao tunaonekana kuwa wasaliti si wasaliti, bali tunachofanya ni kukiimarisha chama, na kuifanya Serikali itimize wajibu wake kwa wananchi.

“Hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ndiye Baba wa CCM, aliwahi kusema wana-CCM wasisite kukosoana na kusahihishana, sasa kosa letu hapa ni lipi? Hivi tangu lini kukosoana kukakidhoofisha chama?

Madai ya kununuliwa na Lowassa:

Kuhusiana na madai kuwa yeye pamoja na wabunge wengine watatu walinunuliwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ili kushiriki harambee mkoani Iringa hivi karibuni, alisema yote hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuchafuana.

Alisema hata kelele zinazoendelea ndani ya vikao vya wabunge wa CCM, kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na hatua yake ya kwenda Iringa, na kampeni hiyo ambayo ameiita ‘chafu’ amesema inaongozwa na Mbunge mkongwe wa chama hicho (jina tunalihifadhi).

“Hivi kweli mtu mzima mwenye akili zake timamu anaweza kudhani au kuamini kuwa Lowassa alininunua kwenda Iringa? Hivi mimi Lugola naweza kununuliwa kwa shilingi ngapi?

“Hizi ni njama za kunivunjia heshima mbele ya wapiga kura wangu na Watanzania kwa ujumla. Wanaonifahamu vizuri wanajua hilo haliwezekani hata siku moja.

“Halafu hawa wanaotoa madai kama hayo, basi wangekuwa wanauliza kwanza au kufanya utafiti kidogo, lakini badala yake nadhani mtu anasinzia na kuota, kisha akiamka anaanza kuzungumza kile alichokiota.

“Ukweli ni kwamba, aliyenialika kwenda Iringa ni Mheshimiwa Filikunjombe ambaye ni mmoja wa wabunge wa mkoa huo, na hili la wabunge kualikana ni jambo la kawaida kabisa.

“Pia tulichokifanya ni kutekeleza dhana ya Mheshimiwa Spika, ambapo aliwahi kusema Bunge linakuwa moja kwa wabunge kushirikiana.

“Ndio sababu mara nyingi tu tumekuwa tukiona wabunge wakialikana majimboni kwenye hafla mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo na kudumisha umoja miongoni mwetu.

“Watanzania wanapaswa kufahamu tukio la Iringa lilikuwa la kiroho na si kisiasa, na mimi ni muumini wa kanisa la Full Pentecostal Church of Tanzania (FPCT).

“Mbali ya kuwa muumini wa FPCT, lakini pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya kanisa hilo, na mke wangu ni mzee wa Kanisa, kwa hiyo hakuna cha ajabu kwa mimi kushiriki shughuli ile ya harambee ya ujenzi wa kanisa Iringa.

“Kwa hiyo unaweza kuona madai kuwa nilipewa pesa ili niende Iringa hayana msingi wowote, nilialikwa na Mbunge mwenzangu, na pia nilikuwa katika sehemu ya majukumu yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi.

“Hata Mheshimiwa Samuel Sitta niliwahi kumualika kwenye harambee Arusha, lakini akakosa muda wa kuhudhuria, na badala yake akaja Mkuu wa Wilaya ya Arusha, na si Sitta pekee, nimewahi kualika viongozi wengi tu.”

Katika vikao vya Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vilivyopita, na vinavyoendelea mjini Dodoma, wabunge hao watatu wamekuwa wakiikosoa Serikali katika mambo mbambali yanayohusiana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Hatua hiyo imewafanya kuonekana miongoni mwa baadhi ya wenzao kuwa ni wasaliti, na wanatekeleza matakwa ya wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika kikao cha ndani cha wabunge wa CCM wiki iliyopita mjini Dodoma, wabunge hao walituhumiwa kuwa wanakidhoofisha chama, ambapo baadhi ya wenzao walipendekeza wachukuliwe hatua za kinidhamu, na ikibidi wang’olewe.

Miongoni mwa wabunge wanaodaiwa kusimama kidete kuhakikisha wanachukuliwa hatua ni pamoja na Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde.

Macho na masikio ya Watanzania hasa wana-CCM yanasubiri kwa hamu kuona na kusikia yatakayojiri kwenye kikao kati ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa na wabunge, ili kujua ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya wabunge hao.

Mchunguzi mmoja wa masuala ya kisiasa aliliambia Rai kuwa, pamoja na tuhuma zote dhidi ya wabunge hao machachari, ni ndoto ya mchana kudhani au kuamini kuwa CCM inaweza kuwang’oa kwa sasa, hasa kutokana na upepo wa kisiasa ulivyo nchini.