Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

ITV, Star TV kwanini mnatuonyesha maiti?

Print PDF

MWANGWI WA LYAMBA-LYA-MFIPA
*Museveni naye ni wale wale!
HAKIKA picha za mikutano ya CCM na CHADEMA nilizoziandikia makala wiki iliyopita zimenipa fundisho kubwa nawashukuru wadau wa safu hii walionipigia simu na wengine kuniandikia ujumbe.

Ndani ya wiki hii yametokea makosa mengine kadhaa katika uchaguzi wa picha za kutumia ama katika magazeti au kwenye runinga; na ni bora nazo tuzizungumzia.

Kuna ajali ilitokea Ngara, Kagera ambapo basi la abiria la Burundi lilimgonga mwendesha pikipiki na kumuua. Siku chache baadaye ajali ya radi ilitokea tena Ngara na kumuua mwanafunzi.

Picha za maiti hawa zilionyeshwa kwenye runinga zetu kama sikosea ni ITV na Star TV! Hapo ni lazima tukubaliane kuwa kuna uchaguzi mbovu wa picha za kutumia unaokwenda kinyume cha taaluma na hata maadili ya uandishi wa habari.

Watangazaji wa vituo hivi vya runinga eti huanza kwa kuwaomba msamaha watazamaji kuwa picha zitakazoonekana kwenye taarifa husika ni za kutisha! Sasa sijui huwa wanataka watazamaji wafanye nini? Waondoke kwenye runinga au wazime kwanza runinga zao ili picha hizo za kutisha zipite?

Kwa kawaida taarifa za habari huwa wazi kwa kila mtu, yaani mzee, kijana na hata watoto wadogo bila kuangalia umri wao. Sasa iwapo kuna picha za kutisha, mnataka wazazi wawafukuze watoto wao sebuleni?

Ni lazima watayarishaji wa vipindi hivi wawe wanafahamu jamii gani au ni watu gani wanaosubiri kutazama taarifa hizo za habari na hivyo waandae picha zenye kuenenda na maadili ya jamii husika huku maadili ya uandishi wa habari yakiwekwa mbele.

Kabla ya kuandika makala haya nilizungumza na waandishi wa habari waliobobea na ambao ni waalimu wa fani hii; Balinagwe Mwambungu na Mwalimu Dk. Ayub Rioba na wote walikubaliana nami kuwa hakuna ‘excuse’ ya kuonyesha maiti, hasa zilizoharibika, kwenye gazeti au runinga. Ni kinyume cha maadili na inakera sana.

Mwanangu anaitwa Zidane, ana miaka mitano. Yeye akiniona tu nimerudi nyumbani huwa anauliza; “baba, saa mbili tayari?” nikimwambia ndio, basi hata kama alikuwa anatazama Kirikou, atazima na kuweka ITV kwa ajili ya taarifa ya habari.

Taarifa za kitaifa zikiisha anabadilisha mwenyewe kwenda Star TV na hapo hatoi hadi BBC imalizike saa tatu na nusu na muda huo mara nyingi huwa ameshalala.

Lakini zile taarifa za kitaifa huwa tunatazama pamoja na mara kwa mara huwa anauliza maswali. Sasa mtoto kama huyo utamwondoa vipi sebuleni ili kupisha kwanza picha za kutisha za maiti walioharibika au kugongwa na magari?

Kwanini hatujifunzi kwa wenzetu ambako hakuna hata maiti mmoja aliyeonyeshwa wakati wa milipuko ya Boston na hata pale WTC ilipolipuliwa Septemba 11 mwaka ule?

Kuna faida gani kuonyesha maiti? Dk. Rioba aliniambia kuwa picha kama hizo huonyeshwa tu baada ya kufahamu maadili ya jamii inayotazama runinga hiyo; pili umuhimu wa picha hizo katika kuipa uzito habari husika.

Sasa maadili ya Watanzania (wote) yanaruhusu kutazama maiti hata kama hazijaandaliwa? Maiti za majambazi, vibaka waliochomwa moto, watu waliokufa kwenye ajali kama yule aliyeonyeshwa na Channel Ten kwenye ghorofa lililoporomoka Mtaa wa Indira Gandhi, wana umuhimu gani katika kuipa nguvu taarifa husika?

Hebu tuuthamini utu wetu jamani na kuziheshimu maiti zetu. Wazungu ambao huwa tunawaiga katika mengi, huwa hawaonyeshi hovyo maiti zao.

Ni aibu kwa wanataaluma kama sisi kufanya uchaguzi mbovu wa picha kwenye vyumba vyetu vya habari ingawa pia ni aibu kwa ma-PRO kufanya hivyo hivyo kwenye ofisi zao kama Ikulu, ofisi za vyama vya siasa na hata kwenye kampuni wanakofanyia kazi.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, mmoja kati ya marais waliopendwa na kukubalika sana na ‘kizazi chetu’ alipoingia madarakani Januari 29, 1986, naye alianza kuonyesha dalili za kuchoka.

Museveni aliingia madarakani akitokea msituni na kumpindua Jenerali Tito Okello na alipoapishwa, mara moja akatangaza mapinduzi ya kisiasa na kiuchumi ndani ya Uganda akisema kuwa wanaodhani kuwa kuapishwa kwake ni jambo la kawaida tu, wamekosea, kwani huo ulikuwa ni mwanzo wa Uganda mpya.

Kamanda huyo aliyezaliwa mwaka 1944, alifanikiwa kuitangaza vyema Uganda iliyokuwa imepitia vipindi vigumu vya vita na kuifanya ikubalike kimataifa, huku uchumi wake ukikua, lakini aliporuhusu vyama vingi, ikawa mwanzo wa kuporomoka kwa sifa zake.

Alianza kwa kumtendea ‘ukatili’ daktari wake wa zamani aliyegeuka kuwa mpinzani wake mkubwa kisiasa, Dk. Kiiza Bessigye. Baadaye akajikuta akilaumiwa na jumuiya ya kimataifa kwa kushirikiana na Rwanda kuendesha vita mashariki mwa DRC.

Baadaye alibadili katiba ili aweze kugombea urais kwa mara ya tatu na tayari kuna kila dalili kuwa atataka kugombea kwa mara ya nne na kuwa mmoja kati ya viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi Afrika.

Sasa majuzi, safu yake ya wataalamu wa habari na propaganda wakaruhusu magazeti kutumia picha iliyomwonyesha kijana mmoja akiwa ameelemewa na uzito wa kiroba cha fedha alichopewa na Museveni! Jamani?

Ati fedha hizo (dola 100,000, sawa na Sh milioni 163) ni kwa ajili ya kikundi kimoja cha vijana kiweze kujiendeleza! Kweli kuna haja ya Rais kutembea na viroba vya fedha kwenda ‘kuwahonga’ wananchi wake? Huu sio udhalilishaji? Alishindwa vipi kuwapa hundi (cheque) vijana hao?

Lakini hapa kosa ni kwenye uchaguzi wa picha. Hata kama Rais amefanya ‘kosa’ hilo (mkubwa hakosei) bado PRO wake angeweza kumshauri kuwa picha hiyo isitumike kwani itazua mijadala rasmi na hata mijadala ya chini chini.

Udhalilishaji kama huu niliwahi kuuona miaka michache nyuma pale msafara wa kifahari wa Rais Muammar Ghadafi ulipokuwa ukitoka Msumbiji kwa njia ya barabara kwenda Malawi.

Njiani rais huyo alikuwa akigawa dola za Marekani kwa ‘masikini’, raia wa Malawi waliokuwa wamejipanga barabarani.

Hizo ni dalili za ‘kufilisika’ kisiasa kwani wakati Museveni akitaka huruma za wananchi wake kwa kugawa viroba vya fedha ili apite kwenye uchaguzi wa mwaka 2016, Ghadaffi alikuwa akitaka ‘urais’ wa Afrika (United States of Afrika).

Maoni  

 
0 #1 da vinci 2013-05-07 10:56
SAWA BOSI WEWE NA MWANAO PICHA HIZO HAMZIHITAJI ILA IPO JAMIII INAZIHITAJI, MFANO WAFIWA, NDUGU NA JAMAA WANAZIHITAJI SO NI WEWE MWENYEWE KUAMUA KUANGALIA AU KUACHA KWANI HULAZIMISHI NA NDO MAANA UKAPEWA TAARIFA KABLA YA KUONESHWA KWA PICHA HIZO ILI UCHAGUE LA KUFANYA.
Nukuu
 

Toa Maoni


Waliotutembelea