SIKU chache baada ya wafanyakazi wa Kampuni ya Said Salum Bakhresa, kutoa malalamiko kuhusu unyanyaswaji wanaofanyiwa , tuhuma nyingine zimezidi kuibuliwa. Tuhuma hizo zinakihusu kiwanda cha kutengeneza mikate kilichopo eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam. Wakizungumza na RAI wafanyakazi hao na wengine ambao wamedai kufukuzwa kazi kwa ajili ya kutetea maslahi yao walisema kiwanda hicho kinaendeshwa kibabe.
Walisema Meneja wa Azam Bakeries, Suleiman Mbacha, ndiye kinara wa unyanyasaji huo huku wakidai kuwa mmiliki wa kampuni hiyo (Bakheresa), hana tatizo.
“Tatizo ni kwamba Mbacha anajua kuwa hatuna uwezo wa kuonana na tajiri (mzee Bakhresa) mwenyewe ndio maana anakuwa anafanya maamuzi kama anavyotaka yeye,” alisema mfanyakazi wa zamani wa kampuni hiyo, Mustafa Said.
Kijana huyo aliyefanya kazi kiwandani hapo kwa zaidi ya miaka saba, alisema ajira yake ilikoma ghafla siku chache baada ya Bakhresa kutembelea kiwandani hapo mwaka jana.
“Alipokuja aliitisha mkutano na tulimweleza wazi kwamba mishahara na posho tunazolipwa ni ndogo sana. Mwenyewe aliliona tatizo hilo, pale pale akaagiza kuwa vibarua wapandishiwe posho kutoka Sh 4,500 kwa siku hadi Sh 6,000, na sisi tuliokuwa tukilipwa Sh 150,000 kwa mwezi akasema tulipwe Sh 200,000,” alisema Mustafa.
Mustafa alieleza kuwa baada ya agizo hilo vibarua waliongezewa posho siku hiyo hiyo isipokuwa yeye na mfanyakazi mwingine Salum Penza ambao walionekana kuwa vinara wa hoja hiyo.
Hata hivyo alisema baada ya kutokea hali hiyo walilazimika kumuona Mhasibu Yusuf Baalawi, na kuhoji sababu ya kutoongezewa mishahara, ndipo walipojibiwa kuwa meneja yaani Suleiman Mbacha amekataa kuidhinisha.
“Meneja aligoma kwa makusudi kwa kuwa eti tulikuwa na kiherehere na matokeo yake akaanza visa hadi akatufukuza kazi,” alisema.
Kwa muda wote aliofanya kazi kiwandani hapo Mustafa hakuwahi kuingiziwa fedha kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Pamoja na malalamiko hayo Mustafa alisema kampuni hiyo ilikuwa imemfungulia akaunti mbili za malipo ya NSSF, jambo ambalo linamshangaza.
RAI ilishuhudia kadi hizo za NSSF Tawi la Temeke zenye namba 37 543 326 iliyofunguliwa Agosti 2, 2006 na nyingine 38 328 313 ya Machi 30, 2007.
“Nilipofukuzwa kazi nilikwenda NSSF nikaambiwa kuwa kadi ya kwanza haitambuliki kwa hiyo haikuwa na michango yoyote isipokuwa kadi ya pili. Kwa maana hiyo miaka minne ya kwanza nilifanya kazi bure bila michango yangu kuingizwa NSSF.
Mustafa alisema kwamba ameamua kuyaweka hadharani madhila yanayowakumba wafanyakazi wa kiwanda hicho chini ya meneja huyo ili kuwasaidia wafanyakazi wanaoendelea kufanyakazi kwenye kiwanda hicho.
Alipotafutwa Mbacha ili azungumzie tuhuma hizo, alikanusha kila kitu na kudai kuwa rekodi sahihi za wafanyakazi pamoja na mambo mengine zipo kwenye Idara ya Uongozi (administration) ya kiwanda.
“Ni uzushi mtupu. Ninakushauri uende utawala na kuuliza, utapata ukweli wa mambo,” alisema Mbacha.
Wafanyakazi wengine ambao majina yao (tunayahifadhi), wamemuomba mmiliki wa kampuni hiyo kuyafanyia kazi malalamiko ya wafanyakazi ili kurejesha amani ambayo inazidi kutoweka kiwandani humo.
Wiki mbil zilizopita, wafanyakazi wa kiwanda hicho walifika kwenye ofisi za RAI kulalamikia unyanyasaji wanaotendewa na uongozi wao.
Miongoni mwa malalamiko yao ni maslahi duni na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa viongozi hao, huku wakiwapendelea zaidi wageni hasa kutoka Kenya na India.
Wafanyakazi hao walisema hali wanayokumbana nayo kazini kwao si ya kuridhisha na kuomba msaada kwa serikali.
Mmoja wa wazee waliofanya kazi kiwandani hapo kwa zaidi ya miaka 15 alisema pamoja na makubaliano ya mshahara wa Sh 150,000 walioafikiana na uongozi, huambulia Sh 80,000 tu kwa mwezi bila kuambiwa makato yake yanapelekwa wapi.
Mbali ya wafanyakazi hao malalamiko hayo pia yametolewa na madereva wanaosambaza mikate maeneo mbalimbali jiji hilo.
Wakati Watanzania hao wakikumbwa na dhahama hizo, uongozi wa kiwanda hicho unadaiwa kuwaajiri raia wa kutoka Kenya na India na kuwapa mishahara minono, nyumba za kuishi na marupurupu kadhaa.
Maoni
Raymond Mauki