*Ashangazwa na utajiri wa watendaji, ataka wachunguzwe
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro, Pius Msekwa, amesema fitna na chuki za kisiasa ndio chanzo cha yeye kuhusishwa na ufisadi.
Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa Tanzania Bara, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na Rai mjini Arusha.
Katika mahojiano hayo, alisema amekuwa akisikitishwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimtaja kujihusisha na vitendo vya ufisadi, ikiwamo kugawa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli ndani ya Ngorongoro.
“Kuna baadhi ya wanasiasa miongoni mwao wakiwamo wabunge ambao wamekuwa wakinituhumu kwa mambo kadhaa, lakini lengo kuu ni kunivunjia heshima kwa kunihusisha na ufisadi.
“Nimekuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa vipindi viwili sasa, na maamuzi mengi yanayopitishwa na kutekelezwa, hufanywa kwa mujibu kanuni na taratibu zinazoendesha Bodi ya Ngorongoro.
“Nimetuhumiwa kugawa maeneo kwa watu kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, lakini ikumbukwe kuwa Mamlaka inayo kamati ya zabuni, sasa sijui mimi naweza kuingilia vipi utaratibu huo na kuanza kugawa maeneo.
“Pia ikumbukwe wazo la kuongeza vyumba kwa ajili ya wageni wanaofika Ngorongoro liliasisiwa na Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara katika eneo hilo, ambapo baada ya ziara hiyo, mwaka 2007 ndipo maeneo yakaainishwa.
“Kilichofuata ni kutangazwa kwa zabuni, ambapo kampuni 38 zilituma maombi, na baada ya mchakato mzima, kampuni zilizoshinda zilipewa kazi, na hili linafahamika kwa sababu hata baadhi ya wabunge walionituhumu, nao pia ni wajumbe wa Bodi ya Ngorongoro, kwa hiyo wanafahamu ukweli wote.
“Maadui zangu wanafahamu wadhifa wangu wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo wanadhani kama watafanikiwa kunichafua, basi watamshawishi Rais Kikwete, ili apoteze imani yake kwangu na mwisho wa siku aache kuniteua,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Bodi, alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, ambapo hadi sasa amekuwa katika wadhifa huo kwa miaka sita, Mamlaka hayo yamekuwa na mafanikio makubwa.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongeza pato la Mamlaka hayo kutoka Sh bilioni 17 mwaka 2006 hadi kufikia Sh bilioni 42 kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni, mwaka huu.
Alisema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea eneo maarufu duniani, hatua ambayo imefikiwa kutokana na mikakati madhubuti ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro.
Kuhusu tuhuma za wajumbe wa Bodi kusafiri nje ya nchi kushiriki maonyesho ya utalii kazi ambayo inapaswa kufanywa na menejimenti, alisema ni kweli wamekuwa wakisafiri, lakini hilo linatokana na sera zilizowekwa na bodi za wakurugenzi zilizotangulia.
“Ni kweli baadhi ya watu wamekuwa wakihoji uhalali wa wajumbe wa Bodi kwenda nje ya nchi kushiriki maonyesho ya utalii, lakini utaratibu huo tuliukuta.
“Lakini katika hili labda nizungumzie jambo moja ambalo kwa hakika lilinishangaza, mwaka 2011, Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa agizo kwamba wajumbe wa Bodi wasiende kwenye maonyesho ya utalii, kwa sababu hiyo ni kazi ya menejimenti.
“Jambo la kushangaza, baada ya kutoa agizo hilo, akaagiza Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wawe wanakwenda kwenye maonyesho hayo.
“Kutokana na agizo hilo, gharama za kushiriki maonyesho hayo zikawa kubwa sana, kiasi cha kuleta mtafaruku kwenye hesabu za Mamlaka, na sote tukabaki tunashangaa,” alisema.
Kuhusu tuhuma zinazowakabili baadhi wafanyakazi waandamizi wa Mamlaka hayo, alisema ni kweli baadhi yao wanamiliki mali nyingi ambazo hazilingani na vipato vyao.
Alisema; “Hizo taarifa ni kweli kabisa, kuna baadhi ya mameneja wana utajiri mkubwa, kwa mfano (anamtaja jina), ni juzi juzi tu tumemteua, lakini tunashangazwa na utajiri alionao.
“Nadhani ni wakati muafaka kwa TAKUKURU kufanya kazi yake, wachunguzwe na waeleze hizo mali wamezipataje, na kama ni za halali, basi wabanwe walipe kodi.”
Maoni