Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Bunge lisilo makini hupitisha sheria mbaya

Print PDF

KITENDO cha Serikali kukubali kuirejesha bungeni Sheria ya Mifuko ya Kijamii, ili ifanyiwe marekebisho katika kifungu kinachohusiana na malipo ya mafao kwa wanachama, kinaonesha jinsi Bunge letu lisivyojali jamii na Serikali yenyewe kutokuwa makini.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, kama Wabunge wetu wangekuwa waangalifu, wakajadili hoja zinazoletwa mbele yao kwa umakini, bila kuingiza misimamo ya kichama, tuna uhakika kwamba sheria hii isingepita.

Lakini kama ilivyokuwa katika Sheria ya Katiba, ambapo Wabunge kwa tiketi ya Chama Cha mapinduzi (CCM), kwa kutumia wingi wao, wakakataa hoja nzuri na ya kizalendo, ambayo ilitaka baadhi ya sehemu za sheria hiyo zirekebishwe. Wakaipitisha kwa mbwembwe na vifijo—kana kwamba wao ndio washindi—lakini, pamoja na Rias Jakaya Kikwete kusaini muswada ule kuwa sheria, na kwa kuwaa Rais ni wa wote, pamoja na wanaompinga na wasiompenda, akatumia busara na kuagiza kwamba muswada ule ufanyiwe marekebisho na urudishwe bungeni.

Bunge kama taasisi, kazi yake kuu ni kutunga sheria, lakini pia Bunge linapaswa kuisimamia Serikali kikamilifu, hasa katika utekelezaji wa mambo yaliyo amuliwa na Bunge na mipango yote ya maendeleo. Kama Bunge ni legelege, Serikali pia itakuwa legelege na kulala usingizi.

Sisi tunawashukuru Wabunge ambao walisikia kilio cha watu wanaowawakilisha, hasa kundi muhimu la wafanyakazi na kupeleka hoja bungeni. Hoja hiyo ilizaa Azimio la Bunge lililoitaka Serikali kupeleka Muswada wa Dharura wa Marekebisho ya Sheria Namba 5 ya mwaka 2012, inayozungumzia marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Tunategemea kwamba safari hii, Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wataitazama upya sheria hii kwa makini na kuondoa au kufanya marekebisho ya vifungu vyote ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa.

Kama ilivyoshauriwa na Bunge, baada ya sheria hiyo kurekebishwa mafao ya kujitoa yarejeshwe na pia wanachama waruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yao ya uzeeni, kabla ya kustaafu ili kujiandalia mazingira mazuri baada ya kustaafu.

Lakini, kwa maoni yetu, viongozi wa ngazi za juu wa mifuko ya pensheni, ambao ni wadau wa Wizara ya Kazi na Ajira, washiriki kikamilifu katika marekebisho hayo. Kiisha wafanyakazi, kupitia mabaraza yao, wapitie marekebisho hayo na mifuko ya pensheni ipeleke mrejesho wizarani ili mapendekezo hayo yaingizwe kwenye muswada utakaowasilishwa bungeni.

Kwa njia hii, tunadhani tutakuwa tumepanua uwanja wa demokrasia na ushirikishwaji. Mifuko hii, kwa kweli si mali ya Serikali, ni mali ya wanachama. Hivyo basi, vipengere ambavyo vinampa waziri husika au Hazina, madaraka juu ya mifuko hii viondolewe.

Kwa maoni yetu, bodi za udhamini, ambazo huteuliwa na waziri, ziwe na madaraka kamili ya kuhakikisha kwamba fedha kutoka mifuko hii haichezewi na yeyote. Bodi zifanye kazi kwa uhuru na kwa kuzingatia mwongozo na sheria ya mifuko hii.

Toa Maoni


Waliotutembelea