Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Hatimaye Bunge lazinduka kuwabana wabaya wa Tanesco

Print PDF

Huenda yule Mbunge machachari wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alilielezea hili vizuri zaidi – pale alipotamka kwamba kikao cha Bunge la Bajeti ni msimu mwingine wa kijinga.

Alitamka hayo baada tu ya Wabunge kuanza kuijadili bajeti ya Serikali iliyotangazwa Bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa mwezi uliopita. Wabunge wa chama tawala (CCM) walimzonga sana kwa kauli hiyo, na kauli za ‘mwongozo’ kwa Spika zilisikika sana Bungeni.

Lakini alichokisema Mbunge huyo hakikuwa mbali sana na ukweli halisi na wananchi tumeona na kusikia mengi kutoka jengo hilo ambalo moja ya kazi zake kazi yake kubwa ilipaswa kuwa ni kutunga sheria, ingawa kwa muda mrefu imekuwa kama mhuri tu wa watawala – kusimamia na/au kupitisha kile watakacho.

Miezi kadha iliyopita niliandika makala katika safu hii kulielezea suala hili na kimoja nilichokisema ni kwamba tukilinganisha, kwa mfano, na Bunge la Uingereza (House of Commons), hili letu la Dodoma limejaa anasa nyingi kama vila wabunge kuketi katika viti vya bembea ambavyo vina uwezo wa kugeuka huku na kule, wakati mwingine baadhi ya Wabunge huamua kukaa mikao ya pembe-mraba (right angle) na Spika. Katika Bunge la Uingereza Wabunge hukaa kwenye mabenchi tu mara nyingine wakibanana iwapo kikao kitavutia Wabunge wengi.

Nilisema ni vigumu hili kutulia akilini—kwamba sisi Watanzania, ambao daima dumu hutembeza bakuli la ombaomba kwa hao hao Waingereza waliotutawala ili watupe pesa tuweze kutunisha bajeti zetu na hivyo kutuwezesha kuishi, tunaweka jeuri ya kuwapiku katika masuala ya anasa ndani ya Bunge? Tena Bunge ambalo kwa bahati mbaya na majonzi makubwa kazi yake kubwa ni kupiga mhuri chochote kile serikali inachotaka au inachokisema?
Iwapo Uingereza, nchi ambayo ukubwa wa uchumi wake ni mara laki kadha kuliko ule wa Tanzania hawajaona umuhimu wa kujenga Bunge jipya la kisasa la kila aina ya anasa inayoweza kufikiriwa, inakuwaje sisi, masikini wa kuombaomba tunafanya anasa kama hizi?

Lakini tukirudi kwa kauli ya Mbunge Lissu ya ‘Bunge la Bajeti ni msimu mwingine wa mambo ya kijinga’ aliyoitoa wakati akichangia mjadala wa bajeti na baada ya kuona Wabunge wa CCM wakiidhihaki kwa kuikejeli Bajeti mbadala ya kambi ya Upinzani Bungeni.

Akifafanua, Lissu alisema kauli yake inatokana na namna serikali inavyoleta vitu Bungeni na Wabunge wanajadili na wengi wanaunga mkono wakati inajulikana wazi kuwa vitu hivyo havitekelezwi.

Alisema kujadili vitu ambavyo havitekelezwi ni “kujidanganya wenyewe, kudanganya watoto wetu na kuidanganya nchi hii, hivyo ni aibu kwetu na kwa wabunge wote (Bunge zima).”

Alitolea mfano wa namna serikali ilivyoahidi katika mkutano wa bunge la bajeti la mwaka juzi kuwa wataweka Tsh8.6 trilioni kila mwaka kwa ajili ya bajeti ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Alisema wabunge walipongezwa sana hata na Rais lakini katika bajeti ya mwaka jana mpango huo ukatengewa Tsh4 trilioni tu na walipohoji inakuwaje punguzo hilo wakajibiwa kuwa ni mwaka wa mpito lakini itaanza rasmi mwaka huu.

Lakini, aliongeza Lissu, mwaka huu tena mpango huo bajeti ya maendeleo imetengewa Tsh4.5 trilioni tu badala ya trilioni 8.6 kama ilivyoahidiwa, hivyo Serikali ilijua kabisa ilikuwa inalidanganya hivyo.

Aidha a alisema mara kadha serikali ilikuwa inaahidi Bungeni kwamba itaziba mianya ya ukwepaji kodi, itapunguza misamaha ya kodi n.k. lakini lugha hizi zimekuwa za siku nyingi sana na zinachosha.

Kwa vyovyote vile hiyo ni tafsiri moja ya Bunge letu sasa hivi. Lakini kuna hali nyingine hasi inayojitokeza kutoka Bungeni siku hizi – ufisadi kutinga Bungeni.

Yumkini hiki kitu si kipya lakini ni mara ya kwanza kinabainika na kuzungumzwa waziwazi bungeni, tena kutoka kwa Wabunge wa pande zote mbili – wa Serikali na Upinzani.

Na ninavyozungumza haya, tayari Mbunge mmoja wa Bahi, Omar Badwell (CCM) ana kesi ya jinai mahakamani kwa kupokea mulungula kutoka afisa wa Serikali.

Cha kusisimua zaidi ni kwamba Mbunge huyu ambaye ni mtendaji kutoka Mhimili wa Kutunga Sheria (Legislature) anadaiwa kupewa hongo na mtendaji kutoka Mhimili wa Utawala (Executive). Kwa maana nyingine Mihimili hii miwili muhimu ya Dola imejikuta katika mpambano, ingawa siyo kwa namna inavyotarajiwa, na shauri limepelekwa kwa Mhimili wa tatu kwa uamuzi – Mhimili wa Mahakama.

Kama nilivyosema ‘mpambano’ huu siyo wa aina iliyotarajiwa kwani umetokea katika ngazi za chini. Lakini katika ngazi za juu, hali si shwari kamwe ingawa Mhimili wa Mahakama haujaingizwa. Wabunge wanatuhumiana wenyewe kwa wenyewe kwa ufisadi, tena kwa waziwazi kabisa na hata kutajana kwa majina.

Wiki iliyopita Spika Anne Makinda aliivunja Kamati ya Nishati na Madini kwa madai kwamba wajumbe wake walikuwa wanapokea milungula kutoka kwa watendaji wakuu wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini – Tanesco na wafanyabiashara wengine, hususan wale wenye kufanya biashara na Tanesco.

Isisahauliwe kwamba Tanesco ni moja ya mashirika makuu ya serikali yaliyobakia ambalo limegeuzwa kama ‘ng’ombe wa maziwa’ anayekamuliwa kwa nguvu zote na watu mbalimbali, hususan viongozi wa serikali.

[Shirika jingine ni Mfuko wa Pensheni wa Jamii (NSSF) ambao tayari unaonyesha kuwa na matatizo makubwa, ila tu huenda bado wakati wake wa mambo kuwekwa hadharani. Hii bila shaka itatokea wakati mmoja wa vigogo atajikuta amenyang’anywa sahani.]

Ingawa sakata la rushwa Bungeni bado halijawekwa wazi kabisa, lakini picha inayopatikana inaonyesha kwamba kuna baadhi ya Wabunge ama wamekuwa na masilahi yao binafsi katika shughuli za shirika hilo la kusambaza umeme, au wanafaidika kwa milungula ili wayatetee makampuni yanayofanya biashara na shirika hilo. Kwa maana nyingine hao ni miongoni mwa wale wanaokuza matatizo yanayolikabili shirika.

Kwa mfano, kung’olewa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando na wasaidizi wake wakuu hakukufurahisha baadhi ya Wabunge, ingawa hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo wakati anawasilisha bajeti yake Bungeni wiki iliyopita, ilieleza kwa kirefu ‘madhambi’ ya uongozi wa Mhando na timu yake katika Tanesco.

Hivyo Prof Muhongo alipata nguvu kwa kiasi kikubwa, kutamka bayana kwamba matatizo ya Tanesco ni ya kupikwa tu na hapohapo kutangaza hakuna tena mgawo wa umeme. Hata hivyo kuisadiki ahadi hii ni katika kufanya subira tu.

Aidha Bunge hili katika kikao chake cha mwezi Aprili kilifanikiwa kuushinikiza utawala kuwaondoa mawaziri kadha, wakiwemo mawaziri waandamizi baada ya kuwatuhumu kwa utendaji mbovu na ufisadi.

Wabunge walisema sasa basi – inatosha hii. Waliona pengine lugha kali ndiyo inaweza kuufanya Muhimili wa Utawala kuchukua hatua. Wakafanya walivyofanya Bungeni.

Wabunge wakaweka kando tofauti zao za kisiasa na kuwa kitu kimoja. Kuna baadhi wanasema kwamba ilikuwa imekubaliwa kwamba ili kutia nguvu na kutaka ujumbe ufike kule kunakolengwa mwanzilishaji Bungeni awe ni Mbunge wa chama tawala – CCM na siyo upinzani. Waliona Mbunge wa upinzani angepuuzwa tu na pengine kuzomewa na wale wa CCM ambao ndiyo wengi.

Hebu fikiria angekuwa ni Lissu au Wenje ndiyo kaanzisha suala hilo Bungeni, nadhani isingefika mbali. Tuliona kilichotokea baada tu ya Mbunge wa Ludewa (CCM) Deo Filikunjombe kutamka kwamba mawaziri wote ni wezi tu.

 

Toa Maoni


Waliotutembelea