*Mkakati mzito wapangwa, wanyama wauawa makusudi
*DC wa kwanza wa iliyokuwa Wilaya ya Masai azungumza
WAKATI vuguvugu la kupinga hatua ya Serikali kuligawa Pori Tengefu la Loliondo likiendelea, taarifa za kuwapo mpango wa uvamizi katika eneo la uwindaji wa kitalii zimebainika.
Vyanzo vya habari kutoka kwenye duru za vyombo vya usalama wilayani Ngorongoro zimeliambia Rai kuwa, baada ya Serikali kutangaza kuligawa eneo hilo, baadhi ya wakazi wake waliandaa mkakati wa kuvamia eneo linalotumika kwa ajili ya shughuli za uwindaji wa kitalii.
Katika hatua hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilitangaza kuligawa eneo la Pori Tengefu Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,000.
Serikali ilisema kilometa za mraba 2,500 zitatumika kwa ajili ya shughuli za kibinadamu kama makazi, ufugaji, kilimo na nyinginezo, na nyingine 1,500 zitabaki mikononi mwa Serikali kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.
Chanzo chetu kilisema; “Wiki iliyopita tulipata taarifa za kuwapo mpango wa kuingiza silaha kutoka nchi jirani kwa ajili ya kufanya uvamizi katika eneo linalotumiwa na mwekezaji kwenye uwindaji wa kitalii.
“Unajua wakazi wa hapa (Wamasai) wana uhusiano wa karibu na kindugu na wenzao wa nchi jirani ya Kenya, kwa hiyo kutokana na mwingiliano uliopo, ni rahisi kwa wahalifu wachache kupenyeza silaha.
“Baada ya kupata taarifa hizo, tulijipanga na kuanza kufuatilia kwa ukaribu, lakini inawezekana taarifa zilivuja, hivyo waliokusudia kufanya hivyo hawakutokea, lakini tupo macho kuhakikisha usalama katika eneo hili.
“Lakini pia kuna mambo mengine ambayo yanafanyika baada ya tangazo la Serikali ambayo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi. Mifugo imepelekwa kwa wingi sana kwa makusudi kabisa, ili kuichokoza Serikali.
“Wanajua wakifanya hivyo na hatua zikachukuliwa dhidi yao, basi watakuwa wamepata sababu ya kuanza kupiga kelele kuwa haki za binadamu zinavunjwa, kwa kweli kuna tatizo kubwa.
“Sasa jambo baya zaidi, taarifa zilizopo ni kuwapo kwa mpango wa kuua wanyamapori bila sababu yoyote ya msingi, wiki mbili zilizopita wameuawa tembo wawili kwa risasi karibu na kambi ya Kleins (kampuni inayojihusisha na utalii wa picha), lakini kila mtu akiulizwa anasema hajui.
“Jambo la msingi linalopaswa kufanyika hivi sasa ni kuhakikisha eneo lililogawanya linawekwa alama za mipaka, ili ijulikane kisheria kuingia ndani yake na kufanya shughuli yoyote ni makosa kisheria, vingivevyo tangazo la Serikali litakuwa halina maana yoyote ile.
***Mkuu wa Wilaya mstaafu azungumza:
Mbali ya kuwapo kwa taarifa hizo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Masai kabla ya kugawanywa na kuzaa wilaya za Monduli, Longido na Ngorongoro kati ya mwaka 1961 na 1967, Mzee Peter Kateto ole Kashe (92), amesema mgogoro wa ardhi Loliondo unakuzwa na kundi la watu wachache.
Akizungumza wakati wa mahojiano, alisema kuna viongozi wachache wa kisiasa ambao wanatumiwa na baadhi mashirika ya nchi wafadhili kuchafua hali ya hewa katika eneo hilo ambalo ni hazina kubwa katika tasnia ya uhifadhi.
“Hapa kuna watu wachache sana ambao wanapewa fedha na Wazungu kwa ajili ya kutuvuruga, ndio sababu unawasikia leo wapo Dar es Salaam, kesho unawasikia wapo Dodoma.
“Lazima tuwahojia na watueleze fedha wanazotumia kuvuruga wananchi na kupambana na Serikali wanazitoa wapi, na wanafanya yote haya kwa masilahi ya nani, lazima wafahamu na kutambua Loliondo si ya Wazungu bali ni ya Watanzania.
“Kama kuna tatizo, si kazi ya watu kushawishi wengine wafanye fujo, badala yake ni kukaa na Serikali na kuzungumza, kwa sababu naamini hakuna nia mbaya katika hili.
“Pia mifugo kutoka nchi jirani ya Kenya imekuwa ni tatizo kwa muda mrefu, lakini sisi wenyeji tumekubaliana kupiga marufuku kabisa mifugo kutoka nje ya Tanzania kuja na kufanya uharibifu wa mazingira,” alisema.
Mzee Kashe alisema tatizo jingine kubwa ni ongezeko la idadi ya watu katika eneo hilo, tatizo ambalo halikuwapo kipindi cha nyuma.
Alisema tatizo la ongezeko la watu linatokana na familia nyingi kupanuka, muingiliano wa wageni ambao si wazaliwa wa Loliondo na sababu nyinginezo, wakati ukubwa wa eneo haujawahi kuongezeka.
“Miaka 20 kurudi nyuma eneo lote lenye mgogoro hapakuwapo watu na mifugo kama ilivyo sasa, kwa hiyo hili nalo linapaswa kutazamwa,” alisema.
Maoni
*Ifike mahali sasa watanzania yaani watendaji wa serikali pamoja na watendwa wananchi tuwe na UTU maana hakika inaonekana ELIMU haimkombowi mtanzania wa chini.
Tukiwa na utu hatutajaribu kamwe kuupindisha UKWELI.
Lazima wauwawe, bora wanyama wasiwepo ili wananchi waliowengi wafaidi maslahi ya ardhi yao.
By the way, serikali lazima ifute amri yake na si vinginevyo. Kuna tetesi kuwa hilo litatokea hivi karibuni.
Victory will be with us soon!!