Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Vyama vya wafanyakazi vimepoteza muelekeo

Print PDF

VYAMA vya wafanyakazi nchini vimepoteza mwelekeo kwa kuwa tangu kuigawa iliyokuwa Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) na kuunda vyama vya kisekta, wafanyakazi nchini hawana vyama vyenye nguvu vinavyoweza kujenga hoja na kutetea wanachama wao ili waweze kupata maslahi bora zaidi.

Hata ilipoundwa Trade Union Congress of Tanzaania (TUCTA), hakuna mabadiliko ya kimsingi ambayo yamefanywa—mwelekeo umekuwa ni ule ule wa viongozi kujiona kwamba wao ni sehemu ya mfumo wa utawala. Ndio maana wameshikilia mfumo na utaratibu ule ule wa kuwaalika viongozi wakuu wa nchi kuwa wageni rasmi kwenye sherehe zao.

Vyama vya wafanyakazi ni vyama vya mapambano, si vyama vya kuwabembeleza waajiri wawape maslahi bora wafanyakazi wao. Wafanyakazi wanapaswa kudai mishahara bora na marupurupu mengine kwa sababu wamewekeza nguvu zao na ujuzi wao kumfanyia kazi mwajiri.

Kwa maoni yetu, vyama vya wafanyakazi kisekta vijitazame upya, viangalie ni vyama vipi vya kisiasa ambavyo vinaweza kutetea maslahi yao na viwekeze kwa maana ya kuwa wadau wa chama hicho kwa kuunganisha nguvu. Kwa hiyo wakati wa uchaguzi, ni wazi kwamba wafanyakazi watakipigia kura chama ambacho kitakuwa kimebeba ajenda yao.

Bila kufanya hivyo tusitegemee kwamba iko siku wafanyakazi wa Tanzania, watashushiwa neema na waajiri wao.

Tumekwishaona kwamba mwajiri yeyote anayezalisha bidhaa, yeye anataka kupata faida kubwa, huku akiwanyonya wafanyakazi kwa kuwalipa ujira kidogo.

Hata wafanyakazi wa Serikali ofisini ambao hawazalishi kwa maana ya bidhaa, huduma wanayoitoa ni kwa lengo la kufanikisha malengo makuu ya Serikali na kwa kufanya hivyo wanastahili pia kuangaliwa vizuri. Maana ni kutokana na watumishi hao, ndio wanaofanikisha malengo na mipango ya Serikali na viongozi wetu wakasimama kwenye majukwaa wakijitapa: “Serikali ya chama chetu imefanya haya, imejenga kile, imeanzisha kile na imetoa huduma ile.”

Jambo jingine ambalo vyama vya wafanyakazi vimeshindwa kulisimamia ni kuendekeza utaratibu mbovu wa waajiri kutowasilisha makato halali ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Jambo hili limekuwa sugu na husabisha usumbufu mkubwa sana kwa wafanyakazi pindi wanapostaafu.

Tulisoma kwenye magazeti jinsi mtumishi mmoja wa Serikali aliyefikia ngazi ya Katibu Mkuu, akisimulia jinsi anavyohangaikia mafao yake na kuzungushwa huku na kule.

Wahusika walipoulizwa wakajibu kwa kiburi kwamba amwona nani? Hakuna haja ya kumwona nani kama utaratibu mzuri wa kuwalipa wastaafu upo na unafanya kazi. Haya ndiyo mambo ya msingi ambayo vyama vya wafanyakazi vyenye kusimamia kidete mambo ya wafanyakazi, vingelikuwa vinapigania—si kwenda kwenye sherehe na kuombaomba. Vinginevyo Mei Mosi, imechuja, haina mashiko, haina maana tena. Kuendelea kusherehekea siku hii ni kupoteza rasilimali na muda.

Toa Maoni


Waliotutembelea