NI dhahiri kuwa wabunge wetu wamechoka kiasi kwamba hawatoi tena mawazo yaliyo makini. Baadhi yao wakiongea wanapwaya tu hasa katika uchangiaji wa kuifanya nchi isonge mbele. Jambo la kusikitisha ni kwamba mbunge anapopewa muda wa kuzungumza husimama bila hoja ya msingi, mpaka dakika alizopewa na Spika humalizika bila kujua alikuwa anachangia jambo gani la muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Bunge letu hivi sasa halitoi msaada wowote zaidi ya kuonyesha mbinga tu, mbinga za Bunge letu hazina maana zaidi ya kupata matunda mabovu.
Si sahihi mbunge kuibuka na kukwamisha kila kitu ili tu ajulikane kwa mbinga zake au chama chake kitwae sifa ya kuendeleza mbinga zisizo na tija. Kwa maana hiyo ni bora wabunge mbinga wajitoe ili nchi ijue mwelekeo ambao utatoa nuru mwisho wa handaki.
Ni muda muafaka wa kuwaelewesha wabunge kwamba, bungeni si shule za vidato wako katika utendaji.
Kuzungumza kwa namna ya kwamba una maneno mengi ya Kiswahili kumpita hata mbunge mwenzio aliyekutangulia hakuvutii kwamba unachangia mawazo ya kuleta maendeleo katika taifa letu.
Zaidi ya hapo ni kuonyeshana nani ana maneno magumu katika lugha ya Kiswahili na katika lugha ya Kiingereza, wakati kiutendaji hamna lolote la maana, bali ni kuwachosha wananchi kwa mbinga zao.
Pamoja na kwamba wabunge hawa wamefikia kikomo cha ni vizuri wakajitambua na kwa ustaarabu zaidi bora wakae kimya.
Wasubiri muda ufike wakapumzike badala ya kujazana ukumbini, na baadaye anaambulia kuzomewa na wananchi.
Hivi sasa mambo yako ukingoni wasifikiri kwamba wananchi hawaoni vituko vyao au wamezubaa, kwa hali jinsi ilivyo wabunge ndio wamezubaa na vyama vyao ambavyo haviwaambii wanyamaze na mbinga zao zisizo na maana yoyote.
Kuna maswali ya kujiuliza Je, ni wabunge au vyama vyao ndio vinavyolifanya taifa lisipige hatua?
Wakati tukitafakari hilo kuna haja kubwa ya wabunge na vyama vyao wajirekebishe kwani taifa litaangamia kutokana na mbinga zao.
Hakuna sababu ya msingi ya kung’ang’ania tu kwamba wote wapo vidato vya sekondari ni lazima kuwe na utofauti.