Rai

  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Serikali yaendeleza ahadi kwa wafanyakazi

Print PDF

SERIKALI imeendeza ahadi zake kwa wafanyakazi nchini kwamba itajitahidi kuyatatua matatizo wanayokumbana nayo na kuboresha maslahi yao kadri inavyowezekana.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) jijini Mbeya jana, Rais Jakaya Kikwete alisema Serikali haiwezi kupandisha ghafla mishahara, bali itafanya hivyo hatua kwa hatua kadri inavyowezekana.

Kikwete pia aliahidi kuwa serikali itakuwa ikikutana mara tatu kwa mwaka na vyama mbalimbali vya wafanyakazi katika harakati za kutatua migogoro, huku ikitengeneza utaratibu wa kukutana pia na waajiri nchini.

“Tatizo la ukosefu wa ajira kwa sasa ni asilimia 12. Kiwango hiki ni kikubwa sana ndiyo maana Serikali inaendelea na programu ya kuwaandalia vijana mazingira ya kujiajiri,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Rais aliwaambia maelfu ya wafanyakazi waliohudhuria sherehe hizo licha ya kuwepo kwa mvua karibu muda wote kuwa sasa mafao ya wafanyakazi yatakuwa yakihamishwa kutoka mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii hadi mwingine kulingana na matakwa ya mwajiri, lakini akatoa wito kwa waajiri kuwaacha wafanyakazi wao wachague mifuko wanayoitaka, kwani kuwachagulia mifuko ni kinyume cha sheria.

Alichukua fursa hiyo kuwaasa Watanzania kuacha mara moja choko choko za udini akisema kuwa vita ya udini kamwe haina mshindi, na kuwaomba waendelee kuifanya Tanzania kisiwa cha amani.

Katika hotuba yake aliyoitua siku kama hiyo mwaka jana, Rais Kikwete aliwaahidi wafanyakazi kuwa Serikali ingepunguza kodi ya PAYE kwenye mishahara yao ili kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi wa kima cha chini.

Kwenye sherehe hizo za mwaka jana zilizofanyika mkoani Tanga, Rais alisema kuwa ukosefu wa ajira ulikuwa asilimia 12 ingawa Serikali yake ilikuwa imefanikiwa kutengeneza ajira mpya milioni 1.2 huku lengo lililowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 likiwa ni kutengeneza ajira milioni moja.

“Kwa ajili hiyo hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kuzalisha ajira mpya nyingi zaidi,” alisema mjini Tanga mwaka jana na kuzitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kufanyika kwa maboresho katika kuendeleza rasilimali watu hasa katika nyanja za elimu, mafunzo na ujuzi na utekelezaji wa mkakati maalumu wa kuwatafutia Watanzania ajira nje ya nchi.

Alisema kuwa hatua hizo zimewezesha vijana wa Kitanzania 1,327 kupata ajira katika nchi za Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Wizara ya Kazi na Ajira mwaka 2011/12.

“Ujumbe wangu mkubwa kwenu wafanyakazi wenzangu ni kuwa Serikali inatambua mazingira ya wafanyakazi na tuko tayari kuchukua hatua ya kuboresha hali hiyo kwa kadri ya uwezo wetu. Hatuwezi kusubiri uwezo uwe mkubwa. Tutaendelea kugawa kilichopo kupunguza makali. Tutaendeleza juhudi za kudhibiti mfumuko wa bei pamoja na changamoto zilizopo. Hatutasita kufanya yale yaliyopo kwenye uwezo wetu,” alimaliza kwenye hotuba yake ya mwaka jana.

Tofauti na mwaka jana wakati wa Mei Mos ambapo mfumko wa bei hasa ya chakula ulikuwa juu, mwaka huu hali ni shwari kidogo na huenda ndio maana Rais hakulizungumzia sana suala hilo.

Lakini wakati akisema kuwa mafao ya wastaafu yatalipwa mara tu baada ya mfanyakazi kustaafu, kumekuwa na malalamiko na tishio la mgomo kwa wafanyakazi kadhaa hasa wa sekta ya elimu wakidai kuwa wapo walimu ambao bado hawajalipwa stahili zao mbalimbali.

Mwaka jana nchi iligubikwa na migomo ya mara kwa mara ya madaktari wakidai kuwekewa mzingira mazuri ya kufanyia kazi.

Toa Maoni


Waliotutembelea