UMOJA wa vijana wa CCM UVCCM ni chombo kilichoundwa kwa minajili ya kuwaunganisha vijana wake wa Tanzania wanaounga mkono sera, siasa na itikadi ya Chma Cha Mapinduzi.
Shabaha za chama kuunda umoja huo ni kuwa shule ya kuandaa wanachama safi na viongozi bora wa CCM. Kwa mnasaba huo, UVCCM utaandaa vijana kuwa raia wema wa Taifa letu na kwamba chombo hiki ni sawa na tanuri la chuma la kuokea makada na viongozi wazuri wa Taifa.
Kwa hiyo umoja huo una wajibu wa kuongeza shughuli zinazohusu maendeleo na maslahi ya vijana nchini, chini ya uongozi wa CCM na unakiri jukumu lake katika historia ya taifa ni kuimarisha umoja wa kitaifa, kuendeleza mapinduzi ya kijamaa, kidemokrasia, mapambano ya ukombozi katika Afrika na dunia nzima.
Umoja wa Vijana wa CCM unatambua kuwa harakati za kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kujenga jamii iliyo sawa na isiyo tegemezi nchini Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla kunahitaji chombo madhubuti kinachounganisha fikra na vitendo vya vijana wote, wakulima na wafanyakazi, wanafunzi vyama vya hiari, wafanyabiashara na vijana wengine kutoka katika sekta binafsi.
Naam hayo ni machache yaliyopo kwenye utangulizi wa kanuni ya jumuiya ya vijana wa CCM, kwa mtu mwenye uelewa kama wangu na maono ya kawaida kama yangu, kwa hakika yaliyoandikwa hapo yanabeba maana kubwa zaidi kwa jumuiya yenyewe na wanajumuiya na kwa chama kilichounda hiyo jumuiya, na yanasadifu uhalisia, lakini yataleta maana zaidi kama kweli yanatekelezeka kwa vitendo na hayabaki kuwapo maktaba kwenye nyaraka tu.
Lakini msingi wa hoja yetu leo nataka tuiangalie jumuiya hii ya chama tawala kwa jicho la tatu, kipindi hiki CCM na jumuiya zake kinafanya uchaguzi wa ndani ya chama wenye lengo la kuunda safu imara kwa ajaili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, na wa Serikali za Mitaa 2014, uimara wa CCM hutegemea sana nguvu na ushawishi wa jumuiya zake kati ya UVCCM na UWT, na hasa UVCCM ambao ni kiungo muhimu kwa CCM kupata ushindi kwenye chaguzi zote.
Kama tulivyoiona historia fupi na malengo mazuri ya UVCCM lakini UVCCM kwa siku za karibuni imekumbwa na mdudu wa watawala na wafalme kuchonga ‘vinyago’ kwa malengo ya kukidhi matakwa yao, kwa maana moja ama nyingine kitendo hiki kwa kiasi fulani kimeupunguzia umoja huu meno ya kung’ata tofauti na UVCCM ya enzi za kina John Guninita, ni kipindi ambacho vijana wa UVCCM walikuwa na meno ya kuing’ata serikali inayoundwa na CCM.
Ni kipindi ambacho taifa zima lilikuwa likitega masikio yake Dodoma kujua nini tena umoja huo utaazimia na utatoka na tamko gani? Kwani misimamo na maazimio ya UVCCM ya wakati huo si tu kuwa yaliitisha serikali na viongozi wa serikali wasio wawajibikaji, bali pia ilikuwa ni jumuiya iliyokuwa na meno makali ya kumng’ata yeyote ambaye alienda kinyume na malengo na shabaha za Chama Cha Mapinduzi pamoja na kwenda kinyume na maadili ya uongozi ndani ya CCM.
Kwa kumbukumbu tu ni kuwa mwaka 1994, John Guninita alikuwa ni Mwenyekiti wa UVCCM, na Katibu Mkuu alikuwa Sukwa Saidi Sukwa, hawa waliokuwa ni wanasiasa vijana wa wakati huo walioonekana ni watu jasiri.
Uongozi wa Guninita ambaye leo hii ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, ulikuwa na ujasiri ambao ni nadra sana kuuona katika zama hizi ambazo UVCCM imegeuzwa na kuwa kijiwe cha vijana wachache wajanja wajanja kujibanza kusubiri U-DC na Ubunge viti maalumu, na huku wakikubali kuwa vinyago vilivyochongwa na kuwatumikia wachongaji badala ya vijana wa CCM.
Guninita akiwa ama ametumwa au kwa kujituma mwenyewe, walikaa na kuamua kufanya kitu ambacho kilimgharimu mno kisiasa. Wao waliamua kuwataja wazi wazi wanachama wa CCM na makada ambao waliamini kwa imani yao walistahili kurithi na kuvaa viatu vya urais vya Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Waliotajwa na vijana hao wa wakati huo ambao kwamba walistahili kuwa wagombea urais kupitia chama hicho, ni Jakaya Kikwete, Dk. Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa na Jaji Mark Bomani. Tamko lao na msimamo huo wa kizalendo na kijasiri usio wa kinafiki ulizua taharuki na tafrani kubwa ndani ya chama chenyewe kiasi kuwa wakajiona wao ni jumuiya yenye meno halisi na wala haitumiki kuwanufaisha wachache wenye maslahi binafsi ndani ya CCM.
Naye muumini mwaminifu wa ujamaa Comrade Kingunge Ngombale Mwiru wakati huo akiwa ndiye Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, aliwakabili vijana wa UVCCM wakiongozwa na Guninita kwamba walikiuka taratibu na kanuni za CCM, kwa kuwa taasisi yoyote ndani ya chama hicho hairuhusiwi kumpitisha mgombe yeyote bila kwanza kupitia katika mchakato wa vikao vya mchujo vya chama kuanzia ngazi ya sekretarieti, kamati kuu halmashauri kuu na kisha mkutano mkuu wa CCM.
Kwa mwaka 2012, ni wagombea wachache sana ambao wamejitosa kugombea wakiwa ni wagombea huru wasiofungamana na makundi hasimu yenye malengo ya 2015. Dhana hii inaufanya UVCCM kuendelea kuwa kiota cha fikra duni na kupoteza ile dhana ya UVCCM kuwa ndio TANURI LA KUOKA VIONGOZI wa nchi.
Kila kijana anayechukua na kurudisha fomu hawachi kuita vyombo vya habari na kurusha kombora kwa kundi hasimu. Kwa maana nyingine hii inaonyesha kuwa kila mgombea tayari ni kinyago kinachochongwa na wafalme na wenye malengo ya 2015.
Hali hii ya wagombea kukubali kuchongwa kama vinyago kwa kiasi kikubwa kumekigharimu CCM na UVCCM, kwani nakumbuka baada ya uchaguzi wa UVCCM 2008, kulifuatia na kazia ya minyukano ya makundi hasimu huku aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM Hamad Yusuph Masauni akiwa moja ya wahanga wa minyukano hiyo ambaye yeye aliishia kujiuzulu kwa madai ya kudanganya umri.
Lakini pia harakati hizo za makundi kunyukana hazikuishia hapo pia zilishuhudia marafiki wawili ambao hawajakutana barabarani Beno Malisa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM na Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM, Pwani na mjumbe wa kamati ya utekelezaji Ridhiwani Kikwete wakitupana mkono na kuhitilafina, hali iliyosababisha UVCCM kushindwa kuwaunganisha vijana kuwa wamoja na nguvu ya chama. Na kila moja kuamua kundi gani ajiunge nalo kwa ushawishi wa kundi husika. Na kuleta ufa mkubwa kwa CCM hasa kwa kuzingatia umuhimu wa UVCCM kwa CCM kutekeleza majukumu yake kama chama tawala.
Kwa mwaka 2012 tayari zoezi la kuchuka na kurejesha fomu limetia nanga, zaidi ya vijana 180 wamejitokeza kuomba nafasi mbalimbali ndani ya UVCCM,
Wingi wa vijana hao umeleta changamoto na hamasa kubwa na kuonyesha msisimko wa hali ya juu kwa vijana wa chama tawala na kuashiria kuwa “Sasa kumekucha jogoo limekwisha wika Dodoma kwa makada wa CCM kuelekea 2015”.
Najua wazi kila mmoja ametumwa na dhamira ya nafsi yake na kusukumwa na changamoto zinazokikabili chama tawala CCM. Kwa maana hiyo bado sisi wote lengo letu linabaki moja tu. Kutengeneza safu ya uongozi makini wa vijana wa CCM utakaokuwa nguzo muhimu kuelekea 2014 na 2015 katika kuipatia CCM ushindi wa kishindo.
Vijana wa CCM ni lazima kila anayeomba nafasi ndani ya UVCCM awe na dhamira ya kuwawakilisha vijana wanyonge na masikini wa vijjini na mijini ambao ndio watoto wa wenye chama, walio wakulima na wafanyakazi. Kwa maana hiyo ni dhahiri CCM itakuwa imezaliwa upya na kurejesha mvuto kwa vijana kote nchini.
Kwa muda mrefu vijana wazalendo tumekosa nafasi na fursa za kushiriki kuleta mageuzi chanya ya fikra ndani ya chama na kwa Taifa.
Vijana wa UVCCM napenda pia ifahamike kuwa CCM na UVCCM ni moja kati ya (vyama) taasisi pekee za kisiasa barani Afrika ambavyo vimekuwa na muundo bora na wa kipekee unaotoa fursa kwa chama kuwafikia wanachama wake toka ngazi za shina, tawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa na taifa.
Kwa kubainisha hilo ni kwamba mwaka 2010 tumeona namna UVCCM ilivyokuwa na mchango hasi katika kuiletea CCM ushindi wa kishindo, na hii ilitokana na vijana kuacha mila zetu za kukipigania chama na kuanza kujipigania wenyewe na jamaa zao.
Lazima tujue wazi kuwa NJIA YA MAFANIKIO HAIJASAKAFIWA..Huku tukilindwa na historia ya umri wetu wa ujana na historia na mchango wa vijana ulimwenguni katika kuleta Mapinduzi makubwa ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa...
Kwa maoni zaidi na mijadala zaidi Tembelea group ya TANURU LA FIKRA face book