*Wasafiri sasa watatembea na makopo
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, naye kaamua kulonga. Wiki iliyopita, Alhamisi kama leo, aliamua kukandia kitendo cha mabasi yanayosafirisha abiria mikoani kusimama porini na kisha kutoa nafasi kwa abiria kwenda kujisaidia haja kubwa au ndogo vichakani!
Eti kitendo hicho ndicho kilichobatizwa na wasafiri kuwa ni “kuchimba dawa”! Sasa Waziri Mwakyembe amekipiga marufuku kitendo hiki.
Dk. Mwakyembe alisema kuwa kuanzia mwezi ujao (Septemba mwaka huu), basi lolote litakaloonekana limesimama njiani kwa ajili ya abiria ‘kuchimba dawa’, mara ya kwanza mmiliki wake atapewa onyo, asipojirekebisha basi lake litafutiwa leseni!
Alisema “kuchimba dawa” kunamdhalilisha sana mwanamke, ambaye amezaliwa akiwa na umbile la kujisitiri, na pia kunashusha heshima ya wazazi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka abiria wote wajisaidie pindi basi linaposimama kwenye vituo vikubwa vya mabasi. Sawa kabisa!
Wiki chache kabla ya Waziri Mwakyembe kupiga marufuku kitendo hicho, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliliambia Bunge kuwa milango iko wazi kwa mwekezaji yeyote anayeweza kujitokeza kujenga vituo njiani kwenye barabara zote za mikoani.
Waziri Mafuguli alisema hayo baada ya wabunge kumueleza bungeni wakati wa kujadili bajeti ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha kuwa ‘kuchimba dawa’ ni sehemu ya uchafuzi wa mazingira.
Wasafiri kwa sasa wamekwisha kujijengea utaratibu, na utaratibu huo umeota mizizi ambapo wasafiri hushuka kwenye basi au gari wanalosafiria na kwenda ‘kuchimba dawa’ porini au vichakani.
Ni kweli utaratibu huu una ila, lakini mwezi ujao hivyo vituo (vyoo) alivyovitaja Waziri Magufuli kuwa vitajengwa katikati ya mapori yetu, hata kama ni vya kulipia, vitakuwa vimekamika?
Ni kweli safari za mabasi huhusisha watu wa rika zote; wakiwamo watoto, watu wazima, wanaume na wanawake. Mazingira ya porini, ambako wasafiri huenda ‘kuchimba dawa’ hakuna faragha wala stara ya kuwasitiri wanapokuwa wanajisaidia.
Wanawake, wanaume, watoto na watu wazima wanaposhuka kwenye basi, wote hukimbilia vichakani. Sababu wamebanwa na haja. Eti hakuna anayejali. Wote wanaonana! Maana huyu kachuchumaa hapa na yule kasimama, kila mmoja ‘anachimba dawa’!
Mtu mzima anavua nguo, tena hadharani kisha anaanza kujisaidia, huku pembeni yake kuna mtoto au mtu anayetofautiana naye jinsia!
Imesemwa na gazeti moja la mwishoni mwa wiki kuwa wakati mwingine mtu anasafiri na wazazi, wakwe, mashemeji, watoto nakadhalika. Wakati wa ‘kuchimba dawa’ huwa aibu tupu vichakani!
Aidha, ‘kuchimba dawa” kunaathiri uoto, ukuaji na ustawi wa majani na miti, ambayo ni muhimu kwa mazingira, pia kwa chakula cha mifugo na wanyama wengine wanaotumia majani na matumizi mengine kwa wanadamu.
Ni kweli karibu vijiji vyote viko katika mazingira ya porini, ambako wasafiri hushuka kwenye mabasi na kwenda ‘kuchimba dawa’. Baadhi ya vijiji viko karibu na maji, kama vile ya mito, visima nakadhalika.
Haja inayotolewa kwenye majani na ‘wanaochimba dawa’ huzalisha vijidudu vinavyoambukiza magonjwa, yakiwamo yale ya mlipuko.
Wanavijiji hawana mazoea ya kuchemsha maji ya kunywa. Je, afya za wanavijiji zina usalama gani hapo? Tunaachia wenzetu magonjwa ilimradi tufike salama safari zetu!
Zaidi ya hivyo, hata wanaochimba dawa hawako salama. Wachimba dawa wengi hawatumii maji wala sabuni baada ya kuchimba dawa! Mtu anamaliza kujisaidia, anavaa nguo zake na kurudi kukaa kwenye kiti ndani ya basi!
Kuna hoteli mbalimbali njiani, ambazo hutumiwa na mabasi mengi kwa ajili ya abiria kujipatia chakula. “Kwa nini mabasi hayo yasiweke ratiba ya kusimama katika hoteli hizo ili kuwapa fursa abiria wao kujisaidia?” gazeti tajwa hapo juu linauliza.
Yaliwahi kuwapo makampuni ya mabasi ambayo mabasi yake yalikuwa na vyoo ndani, mfano Scandinavia na Fresh ya Shamba, ambako mtu aliposhikwa na haja, alikuwa anakwenda chooni kujisaidia katika mfumo wa kiungwana, kistaarabu na bila shida yoyote. Mabasi haya hayapo tena. Kwanini tusiige mfano huo sasa kwa mabasi yote?
Lakini ni dhahiri kabla hatujajenga vyoo maporini kama ilivyopendekezwa, na kwa kuwa amri ya Waziri Dk. Mwakyembe itaanza kutelezwa kabla ya mabasi hayajawa na vyoo ndani, tutarajie watu kujikojolea nadani ya mabasi!
Kuna wasafiri wazee, kuna wagonjwa wenye matatizo ya vibofu vya mkojo, kuna watoto na wasafiri wengine wenye matatizo mbalimbali, hawa wote hawawezi kuvumilia hadi basi lifike kwenye vituo vyenye hoteli njiani. Hawa watajikojolea ndani ya mabasi.
Sasa kusafiri na makopo ya kukojolea mkojo utakuwa mtindo mmoja, eti?