*Rais Kikwete azima tambo zake
*Atuhumiwa kuvuruga chaguzi UVCC, UWT
*Amtumia Balozi wa Heshima kisiasa
TAMBO za kipindi kirefu za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuwa siku moja atawataja watuhumiwa wa kashfa ya rada zimezimwa.
Membe ambaye ni mmoja kati ya wanasiasa wanaotajwa kuwania uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Juni mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akiahidi kuwataja watuhumiwa bungeni.
Membe ambaye alisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake bungeni Jumatatu wiki hii, alishindwa kutekeleza ahadi yake licha ya kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wabunge.
Kabla ya Waziri Membe kusoma hotuba yake bungeni, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisoma taarifa rasmi ya Serikali, kuhusu sakata la rada, ambapo pamoja na mambo mengine, alisema hakuna mtuhumiwa wa rada anayeweza kupelekwa mahakamani na hivyo kufunga rasmi mjadala huo.
“Hata Uingereza iliyochunguza suala hilo, imeeleza bayana kwamba hakuna rushwa, Serikali haiwezi kumfikisha mtu yeyote mahakamani,” Chikawe aliliambia Bunge.
Kauli hiyo ya Chikawe ilitolewa siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuwaambia wahariri wa vyombo vya habari alipokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwa hakuna ushahidi unaojitosheleza kuwashitaki watuhumiwa.
Rais Kikwete alisema kwamba Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo, kwa kuwa hata Uingereza ilikana kampuni ya BAE Systems kutoa rushwa, na badala yake ikakiri kukosea kuandika hesabu zake.
Alisema ugumu huo, unatokana na mazingira yaliyojengwa nchini Uingereza, yakionyesha kwamba Tanzania haiwezi kupata ushahidi wowote kuhusu suala hilo.
“Sasa hapo sisi tunaanzia wapi, maana kwenye asili ya tukio hili, wanasema hakuna rushwa, kwa hiyo wanasheria wetu tukiwauliza, nao wanahoji kwamba tunaanzia wapi katika suala hili,” alisema Kikwete.
Mara kadhaa, Waziri Membe amenukuliwa akisema Serikali ya Tanzania inapaswa kujisafisha kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa rada na kusisitiza kuwa wapo na wanafahamika.
Alisema kila aliyehusika na kashfa hiyo, ametajwa na kuwekwa picha yake katika kitabu cha, ‘The Shadow World-Inside the Global Arms Trade,’ kilichoandikwa na Andrew Feinstein, ambaye ni mwandishi mahiri nchini Afrika Kusini.
Alisema atawataja kwa sababu kimya chao, tangu kutoka kwa kitabu hicho, kinamaanisha kwamba wanahofia kukanusha, kwa kuwa wamehusika.
Kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Silaha ya BAE Systems ya Uingereza, ilianza mwaka 2000 na imekuwa ikiibuka mara kwa mara.
Ilimfanya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Clare Short, wakati wa Serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair, kujiuzulu, akipinga Uingereza kuiuzia Tanzania, nchi maskini rada hiyo kwa bei kubwa.
Kashfa hiyo kwa muda mrefu pia imekuwa ikitajwa kumhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, ambaye pia aliwahi kukutwa na zaidi ya Sh bilioni 1 kwenye akaunti kisiwani Jersey, fedha ambazo Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ilikuwa ikichunguza kama zilikuwa na uhusiano na biashara hiyo.
Pia kuna kesi ya rada katika Mahakama ya Kisutu, huku Polisi ikiendelea kumtafuta aliyekuwa dalali wa biashara hiyo, Sailesh Vithlan, ambaye anatuhumiwa kushawishi na kuhonga baadhi ya maofisa wa juu na wanasiasa nchini, ili wanunue rada hiyo.
Serikali imeshapokea Pauni 29 milioni za malipo ya fidia kwa Tanzania, na imekubaliwa kwamba fedha hizo zitatumika kununua vitabu na madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.
Aidha katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha ITV, Waziri Membe alitamka kwamba atawataja watuhumiwa wa rada pamoja na wabaya wake wa kisiasa.
Kabla ya kutoa ahadi hiyo, Membe alidai kuna baadhi ya watu wanamfuatafuata kuhusiana na uchaguzi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Wanajua mambo yote haya, wanaogopa nisiwaguse na wangekuwa na uwezo wangeanza kampeni, labda nioteshwe (urais) na ole wao nikioteshwa ndoto hiyo.
“Mtu aliye mbaya wako anakuwa na macho matatu. Kwa hiyo kutokana na uwezo wa jicho la tatu, anaanza kuzuia lile analoliona lisitokee. Mimi nina macho sita. Nitawataja. Hebu wewe fikiria, kila baada ya miezi miwili, naletewa mitego, vituko. Lakini nawaambia Watanzania, waache waseme na mimi ipo siku itakuwa zamu yangu, nitawaweka wazi ili kila mtu aelewe.
“Wasije wakadhani wakijificha kwa wahariri, majumbani kwao ambako ndio kuna ofisi zao, kwenye ma-godown (maghala) yao ndiyo watakwepa, nitawalipua ili wajue. Ukikaa juu ya nyoka, akigeuka atakuuma tu.
“Ipo siku nitawaanika hao watu na wapo kumi na mmoja. Kuna waandishi wa habari mle ndani wawili. Nitawatwanga peupe. Ninyi subirini hata ndani ya Bunge, nitazipangua tuhuma hizo moja baada ya nyingine.
“Nikimaliza bungeni wajiandae, nitawaanika majina yao, picha zao na mambo yote waliyoandika kwenye magazeti kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wangu kwenye wizara,” alisema.
Chaguzi UVCCM, UWT
Wakati joto la uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mikoa na Taifa, likizidi kupanda, Waziri Membe tayari anatajwa kujihusisha na baadhi ya makundi ya wagombea.
Makundi anayotajwa Membe kujihusisha nayo ni yale yanayochuana kuwania nafasi za uongozi kitaifa kwenye Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Miongoni mwa wagombea ambao anatajwa kuwaunga mkono, ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, ambaye anawania nafasi hiyo dhidi ya Mwenyekiti wa sasa Sophia Simba na wagombea wengine saba.
Wakati Membe anasemekana anamuunga mkono mgombea huyo, imeripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa Kilango amepokea kitita cha fedha kutoka kampuni moja ya Kichina kwa ajili ya kufanyia kampeni
Kampuni hiyo ambayo imewa kazi ya ujenzi jijini Dar es Salaam, inadaiwa kutoa kitita cha fedha, ili kuhakikisha Kilango, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge, anachaguliwa kwenye nafasi hiyo.
Habari za kuaminika zinasema Kilango, alianza kazi ya kuwafikia baadhi ya makatibu wa mikoa wa UWT na kuanza kuwashawi, ili wamchague katika nafasi ya uenyekiti kwa ahadi ya kuondoa ukomo kwa Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM.
Taarifa hizo zimesema nguvu ya fedha ilianza kuonekana Machi 13-14 mkoani Dodoma, baada ya kuandaa semina kwa kukusanya wenyeviti wa wilaya na mikoa, waliokuwa wakihudhuria semina elekezi, kuelekea uchaguzi wa ndani na nafasi ya mwanamke katika kuwania uongozi.
Katika semina hiyo, inadaiwa Mbunge huyo, alitumia muda wa jioni kuwashawishi viongozi wa mikoa ili wakati ukifika, wamchague.
Kwa upande wa UVCCM, inadaiwa kuwa Membe tayari anawaunga mkono wagombea watatu (majina tunayahifadhi), ambao wanawania nafasi za kitaifa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika kufanikisha mikakati hiyo, Waziri huyo kwa kushirikiana na Balozi wa Heshima anayewakilisha nchi moja hapa Tanzania, wamefungua ofisi ya kuratibu shughuli hizo maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam, karibu na Kanisa la Mtakatifu Petro.
Pia kijana mmoja, amekuwa akitumiwa kupitia mitandao ya kijamii kuwachafua baadhi ya wagombea, ambapo amekuwa akijitambulisha kwa jina la Mbopo, na pia ni mtumishi wa Serikali.
Maoni
Suala la wagombea sioni kama linawalakini kwake kuwa na mtazamo wa mtu fulani. Hapa hujaeleweka kama unamtuhumu Mh. Kilango au Mh. Membe?