*Wapinzani wamehalalishwa na Katiba kufanya kazi ya kuikosoa Serikali
*Hawatakiwi kuwa wabishi, bali wabainishaji mapengo
TAKRIBANI miaka saba inayeyuka tangu tupate Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Jakaya Kikwete, na kwa mantiki hiyo, tangu Serikali ya awamu ya nne iingie madarakani.
Rais, ambaye anafasiliwa katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu kuwa ni “kiongozi mkuu kabisa wa nchi ambayo ni jamhuri” si mwananchi wa kawaida. Rais ni mwananchi ambaye amepewa madaraka na mamlaka makubwa juu ya nchi husika na watu wake wote.
Anaweza kufananishwa na mkuu wa familia anayetegemewa na wanafamilia wake. Nchi ni familia pana na tata, na rais anaangaliwa au kufikiriwa kuwa mtu anayetegemewa kupanga mipango ya kuwaletea neema watu wake. Kwa hiyo urais ni wadhifa mkubwa, nyeti na wala si kazi ya lelemama.
Baadhi ya watu hujiuliza kwa nini binadamu mwenye akili timamu apende kujitwisha mzigo mzito kama huu, iwe ni katika nchi tajiri au masikini. Umasikini una matatizo yake na utajiri una matatizo yake.
Nchi masikini kama Tanzania, wadadisi wa aina hii huhoji kwa nini mtu apende kugongwa na kichwa kila kuchapo na kuchwapo akifikiria jinsi ya kupambana na umasikini wa taifa na mambo yanayokwenda na hali hiyo.
Vile vile kwa upande wa nchi tajiri, kama vile Japan au Marekani, wadadisi pia huhoji iweje mtu aache kufurahia utajiri wake atake kujigongesha kichwa kila kuchapo na kuchwapo kukabiliana na matatizo ya utajiri.
Kwa mfano, kama si utajiri, leo hii Marekani isingekuwa inapigana vita huko Afghanistan na kwingineko duniani. Kwa ufupi, Rais wa nchi yo yote si mwananchi wa kawaida. Zaidi ya kujitoa mhanga wa kugongwa na kichwa kila kuchapo, wadhifa wa urais huambatana na madaraka na mamlaka makubwa kiasi cha kuyeyusha huo uwangwaji wa kichwa, na mara nyingine kuwafanya walioshika wadhifa huo kujihisi au kufikiriwa na wengine kuwa kama miungu wadogo.
Hisia kama hizi si jambo la ajabu, zinaendana na hulka ya binadamu. Tunajua mifano ya baadhi ya marais waliofikia hatua ya kugeuzageuza Katiba za nchi zao kwa hila au kufanya vitendo vya udhalimu ili wawe miungu wadogo wa maisha.
Si kusudi la makala haya kulijadili suala hili pana na tata, bali lengo kuu ni kujadili uzito wa kauli wazitoazo marais.
Tofauti na wachambuzi wengine wa mambo ya kisiasa na kiuchumi wanaolazimika kusubiri pengine siku 100 au 200 au 300 au hata mwaka, kuanza kuhakiki au kufanya uchambuzi yakinifu wa utendaji wa rais na serikali yake, wachambuzi wa lugha na matumizi ya lugha katika uwanja wa siasa kazi yao huanza mara moja pale mhusika anapokula kiapo cha kukubali wadhifa huo.
Kama nilivyosema hapo juu kuwa rais si mwananchi wa kawaida, vivyo hivyo na maneno au kauli azitoazo huwa hazichukuliwi kijuujuu. Mintaarafu ukweli huu, marais huwa waangalifu sana wanapozungumza katika miktadha rasmi na isiyo rasmi, kwa sababu wanajua hadhira inawasikiliza kwa makini na kulipatia kila neno walitamkalo thamani isiyokuwa ya kawaida.
Neno la kiongozi, kama rais, linaweza kuwa sumu au tunu kwake mwenyewe. Waliowahi kusoma tamthilia ya Kinjekitile iliyotungwa na Ebrahim Hussein ikiwa inaakisi tukio la kihistoria hapa Tanzania, yaani vita ya Maji Maji, watakumbuka pale Kinjekitile, mhusika mkuu, anapoombwa na Kitunda atoe ruhusa ya wapiganaji kwenda kupambana na askari wa Kijerumani.
Kinjekitile ambaye alikuwa Amiri Jeshi Mkuu, alikwisha kuwahakikishia wapiganaji wake kuwa maji yatawakinga dhidi ya risasi za Kijerumani. Anasikika akijisemea kwa mbali: “Binadamu huzaa neno, neno hushika nguvu, likawa kubwa, kubwa, kubwa likamshinda binadamu kwa ukubwa na nguvu.
“Likamwangusha. Neno ambalo limezaliwa na mtu likaja kumtawala mtu yule yule aliyelizaa.” (uk. 33).
Katika muktadha unaoakisiwa na mchezo huu wa kuigiza, Kinjekitile alikuwa Rais wa jamii yake hiyo ndogo. Alisema neno na watu wake wakalipa uzito pengine kuliko yeye alivyokuwa amefikiria.
Wengine hatukuwapo katika sherehe za kumtawaza Rais mpya, Jakaya Kikwete, zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa, Desemba 21, 2005, lakini kwa kupitia vyombo vya habari tuliweza kuona au kufahamishwa jinsi sherehe hiyo ilivyofana sana.
Kati ya mengi aliyoyasema, kuna vipande vya kukumbukwa katika hotuba yake ya kwanza kama Rais, aliyoitoa mara tu baada ya kuapishwa.
Hotuba hiyo ya Rais Kikwete ni mojawapo ya mambo yaliyonivutia, na hususan matumizi ya methali ya Kiashanti, mojawapo ya makabila makubwa nchini Ghana, Afrika ya Magharibi. Hii ilinikumbusha suala la matumizi ya methali na dhima yake katika hotuba au mazungumzo.
Methali ni usemi wa kisanii wa kimapokeo unaofikiriwa na jamii kuwa kweli, na hutumiwa kufumbia au kupigia mfano ukiwa umebeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotutumiwa kukanya au kufundisha hadhira. Kwa hakika, methali huweza kusema mengi katika sentensi moja. Utumiaji wa methali muafaka ni mojawapo ya umahiri katika mawasiliano ya lugha ambayo ni zana kuu ya mwanasiasa.
Rais Kikwete, katika hotuba yake hiyo ya Desemba 2005, akiwa anawaasa wapinzani waungane na Serikali yake kupambana na umasikini, alitumia methali ya Waashanti ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa ni “watu wawili ndani ya nyumba inayoungua moto, hawaachi kuzima moto huo na kuanza kubishana”.
Nimejaribu kuwauliza wazungumzaji wa lugha hiyo wanipe methali yenyewe katika uasilia wake, lakini hawakuweza kuikumbuka. Hata hivyo tunaamini hiyo methali ipo kweli, vinginevyo rais asingeitumia. Mintaarafu methali hii ninataka kujadili mambo mawili, uteuzi wake na maudhui yake kwa kuzingatia muktadha wa hotuba.
Kuhusu uteuzi wa methali, tunaweza kujiuliza kwa nini Rais Kikwete alipiga masafa ya mbali kiasi hicho kusaka methali hiyo badala ya kupekuapekua katika methali za Kiswahili au za makabila ya hapa Afrika ya mashariki.
Jibu ni rahisi. Kwa kawaida mzungumzaji hafungwi kutumia semi au methali za lugha nyingine. Inawezekana hakupata methali ya Kiswahili inayowasilisha vizuri ujumbe aliokuwa amekusudia, au methali ya Kiashanti ndiyo iliyomjia haraka katika kumbukumbu yake.
Kama lugha inayotumiwa na mzungumzaji haina methali inayofaa, basi hicho kinaweza kuwa kichocheo cha kupekua katika lugha nyingine. Lakini kwa kawaida, mzungumzaji atatumia methali ya lugha anayoijua au amewahi kuisikia ikitumiwa na watu wengine.
Uteuzi wenyewe wa lugha au usemi kutoka lugha au jamii nyingine husika huwa ni njia mojawapo ya kuvuta usikivu, lakini pia waweza kuwa umebeba ujumbe wa kijamii kwa kuongezea katika ujumbe wa kimaudhui.
Huwa tunasikia watu wanasema kama Waswahili wasemavyo au kama Waingereza wasemavyo, n.k. Mojawapo ya ujumbe wa kijamii katika uteuzi wa methali ya Kiashanti inaweza kuwa ni kuashiria kuwa mzungumzaji ni mtu asiyejifunga na mipaka ya taifa moja au ukanda mmoja wa bara au dunia hii.
Ni mtu anayekaribisha maoni kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hususan sehemu tofauti za Afrika. Ni mtu wa kimataifa au aliyekutana na watu wa mataifa mbalimbali, au mtandawazi anayeamini kila jamii ndogo na kubwa inaweza kutoa mchango katika jumla ya maendeleo yaliyojikita katika mchakato wa utandawazi, n.k.
Methali yenyewe ni fani iliyobeba maudhui, yaani ujumbe wa kimaudhui. Kwa nini Rais Kikwete alitaka kutoa ujumbe kama huu kwa wapinzani? Tukiichunguza methali hii kwa makini tunaona kuwa ni yenye maudhui ya kibusara, kwamba kama nyumba inaungua, basi waliomo ndani wana wajibu wa kuzima moto badala ya kuanza kubishana.
Baada ya kutamka methali hiyo katika hotuba yake, alifafanua kuwa Watanzania wanakabiliwa na jukumu kubwa la kutokomeza ufukara. Kwa hiyo sitiari (metaphor)ya nyumba katika methali inasimamia taifa la Tanzania, sitiari ya moto inawakilisha umasikini, na watu wawili ni Watanzania.
Sitiari hizi zimetumika kwa usahihi kabisa. Inafurahisha kuona kwamba Rais Kikwete alitambua (bila shaka bado anatambua) kuendelea kusisitiza janga linaloongoza katika kuteketeza taifa, yaani umasikini, na kulifananisha na nyumba iliyoshika moto.
Pia tunaweza kukubaliana naye kwa kuonyesha busara na kusisitiza kuwa kazi ya kuzima moto huu ni wajibu wa kila Mtanzania, awe mwanachama au mshabiki wa Chama Cha Mapinduzi au chama cha upinzani.
Ni kweli kabisa, umasikini kama ulivyo UKIMWI, haubagui katika misingi ya uanachama au imani katika itikadi fulani. Lakini tofauti na UKIMWI, umasikini una tiba mahususi ambayo ni utawala bora. Utawala bora ni mada pana sana na wataalamu wameandika majuzuu (volumes) mengi ya vitabu juu yake.
Kwa muhtasari tu ni kwamba mtawala ndiye aliyeshika kisu na ana mamlaka ya kuwakatia vipande vipande walaji. Kama ukatajikataji huo hautakuwa umetawaliwa na hulka za kiufisadi, basi huo ndio utawala bora, na kila aliyechangia katika kumtunza ‘mbuzi’ huyo atapata haki kulingana na mchango wake.
Hata hivyo, wengine tunaiona methali nzima kama hii haisadifu katika muktadha wa busara za siasa za upinzani. Methali hii inapotosha ukweli wa siasa za upinzani, na kwa kuitumia katika muktadha huu inaashiria mtazamo hasi wa Rais dhidi ya mfumo mzima wa upinzani.
Methali hii inaweza kufasiliwa kama msisitizo wa falsafa ya Kikwete ya utawala bora ambayo alianza kuiibua wakati wa kampeni za uchaguzi wa kuwania nafasi hii kwa mara ya kwanza ambapo alitumia sitiari ya “mafiga matatu”.
Kikwete aliona utawala bora ni kuwa na wabunge na madiwani wa chama chake tu. Kwa hiyo ukijumlisha mafiga matatu na methali ya Kiashanti unapata utawala bila upinzani. Kwa mtazamo mwingine tunaweza kusema huo ni utawala laini. Utawala laini ni utawala wa “ndiyo mzee” na hupendwa na watawala wote.
Kwa hakika upinzani si kubishana na Serikali kwa sababu ya kubishana tu. Inawezekana baadhi ya wapinzani (wakiwamo waumini wa chama tawala – CCM) wameonesha tabia hiyo ya kubishana badala ya kujenga hoja.
Lakini ni bora kubishiwa na ukajikuna kichwa ukijiuliza kwa nini mtu mwenye akili timamu anakubishia kuliko “ndiyo mzee” hata pale ambapo umesahau kufunga zipu ya suruali!
Tukichukua mifano ya mijadala ya bungeni katika Bunge letu, tunawasikia wabunge wa Upinzani wakitoa hoja nzito dhidi ya mipango ya Serikali iliyokuwa ikionekana au kufikiriwa kuleta hasara kwa taifa au kuwanyanyasa wananchi. Baadhi ya hoja zao chache zinazingatiwa na marekebisho kufanyika, na nyingi zinapuuzwa!
Ingefaa kama Rais Kikwete angehimizwa au kuwapa moyo wapinzani kuchokonoa Serikali ili Serikali yake iweze kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa wananchi.
Mwanzoni mwa uongozi wa Rais Kikwete, magazeti yalimnukuu Rais wa zamani wa Zanzibar, Salmin Amour, akikiri kuwa mtu akiwa ndani ya Serikali haoni nyufa na mapengo yaliyomo katika utendaji wake kama yule aliye nje ya Serikali.
Hivyo Serikali ya awamu ya nne isiogope kukosolewa, na baadhi ya wakosoaji waliohalalishwa na Katiba ni wapinzani. Vivyo hivyo, wapinzani hawatarajiwi kuwa wabishi, bali wabainishaji makini wa mapengo na nyufa katika mipango ya Serikali na kuyajengea hoja madhubuti.
Ni heri watu wawili ndani ya nyumba inayoungua kubishana kwa muda wa dakika tano ili kugundua chanzo na mbinu za kukabiliana na moto huo, kuliko kuendelea kuzima moto kiholela kwa saa mbili nzima na nyumba yote kuteketea, na mwisho wakabaki wote wametoleana macho!
Serikali ya CCM itatenda kazi zake kwa ufanisi kama kuna mtu wa kuinyooshea kidole, kwa mujibu wa sheria za nchi. Na huo si ubishi wa watu walio katika nyumba inayoungua.